Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema bado hali ya usafi wa miji hapa Zanzibar hairidhishi na inahatarisha afya za wananchi hususani katika kipindi hiki cha mvua.

Wamesema hayo walipokuwa wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya nchi ofisi ya rais Tawala za mikoa, Serikali za mitaa na idara maalum za SMZ.

Wajumbe hao wamesema licha ya wizara kutekeleza shughuli zausafi za maeneo ya miji lakini bado hali ya uchafu inaongezeka hivyo wameitaka Wizara hiyo kuhakikisha waliopewa dhamana wanasimamia kazi zao kwa ustadi mkubwa.

Pamoja na hayo Wawakilishi wamevipongeza vikosi vya SMZ kufanya vizuri katika ujenzi wa majengo ya miradi mbalimbali ikiwemo skuli na masoko hali inayotia matumaini ya uwepo wa wakandarasi wazalendo wenye uwezo mkubwa.