Maafisa nchini Colombia wanasema watoto wanne waliotoweka tangu ndege yao kuanguka msituni wamepatikana wakiwa hai zaidi ya wiki mbili baadae.

Mama yao na watu wazima wengine walifariki katika ajali hiyo.

Shirika la serikali la ustawi wa watoto ICBF limesema limepata taarifa kutoka eneo hilo kwamba watoto hao wangepatikana wakiwa na afya njema.

Wanajeshi wanaoshiriki katika msako huo, hata hivyo bado hawajawaona watoto hao wenyewe.

Ndege hiyo ndogo aina ya Cessna 206 waliyokuwa wakisafiria ilikuwa ikisafiri kutoka Araracuara ndani kabisa ya msitu wa Amazon kusini mwa Colombia kuelekea San Jose del Guaviare ilipotoweka asubuhi ya Mei mosi.

Baada ya msako mkubwa uliohusisha zaidi ya wanajeshi 100 hatimae ndege hiyo ilipatikana jumatatu wiki mbili baada ya kutoweka.

Miili ya rubani, rubani msaidizi na Magdalena Mucutuy (33) mama wa watoto hao wanne ilipatikana katika eneo la ajali katika jimbo la Caqueta.

Lakini watoto hao ambao wana umri wa miaka 13, 9 na 8 pamoja na mtoto mchanga wa miezi 11 hawakupatikana.