Na Muandishi wetu

Walimu polisi 48 wa Mikoa mitatu ya Unguja wanapatiwa mafunzo ya somo la Usalama wetu kwanza, ambalo litakuwa likifundishwa kwa wanafunzi wa skuli za msingi ili kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji.

Akifungua mafunzo hayo ya wiki moja, Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeda Rashid amesema somo hilo litasaidia kuibua taarifa za vitendo vya udhalilishaji ambazo hazijaripotiwa katika vituo vya polisi.

Aidha ameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kuruhusu kutolewa kwa somo hilo katika skuli mbalimbali nchini.

Nae Kamanda wa polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, ACP Richard Mchomvu amesema asilimia 80 ya makosa ya udhalilishaji yanatokana na watoto wenyewe kujiingiza katika mapenzi hivyo wakipatiwa mafunzo hayo itadaidia kupunguza makosa hayo.

Awali Mratibu wa program ya Malezi mbadala kutoka SOS, Nyezuma Simai amesema wameamua kutoa mafunzo hayo kwa walimu polisi ili kuwajengea uwezo wa kufundisha haki, wajibu wa mtoto pamoja na kuvitambua na kujilinda na vitendo vya udhalilishaji.