Na Muandishi wetu

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameiasa jamii kuacha kutelekeza familia kwa kisingizio cha talaka na badala yake wazichunge ndoa zao ili kujenga ustawi wa jamii iliyobora.

Ametoa nasaha hizo kwenye msikiti mkuu wa Ijumaa Malindi, Mjini Unguja alipojumuika na waumini wa dini ya kiislamu kwenye ibada ya sala ya Ijumaa.

Alhaj Dkt. Mwinyi amesema wanawake wengi wanaopewa talaka hutwishwa mzigo wa ulezi wa watoto jambo linalochochea ugumu wa maisha na kusababisha watoto wengi mitaani kuishi kwenye mazingira magumu.

Pamoja na hayo amewaomba waumini kuendelea kuwaombea dua za heri viongozi kwenye jukumu kubwa la kuiongoza Zanzibar.

Naye Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Ali Mfaume ameitaka jamii hususani wanaume kutatua matatizo yao kupitia mafundisho ya mtume SAW badala ya kutoa maamuzi mabaya yenye athari mbaya kwa jamii.

Nae khatibu wa sala ya Ijumaa Sheikh Ali Abdulfatah amesema talaka ni jambo la halali analolichukia sana Allah SW huku akiisihi jamii kuzifuata sheria na sunna za talaka zilizowekwa kwa misingi ya dini.