Waziri wa uchumi wa buluu na uvuvi Suleiman Masoud amesema mashirikiano kati ya Zanzibar na Misri yataleta mageuzi makubwa kwenye mnyororo wa thamani katika sekta ya uvuvi, ufugaji na mazao ya baharini Zanzibar.

Ameeleza hayo katika kikao cha ushirikiano kati ya Wizara hiyo na kampuni ya Evergreen Egypt United National Company for fisheries, Aquaculture na kampuni source link zote kutoka nchini Misri.

Hapo Mei 15/2023  kampuni hizo zilitiliana saini na Wizara hiyo mbele ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi wa makubaliano mbalimbali ikiwemo uletaji na uendeshaji wa pamoja wa meli za uvuvi katika bahari kuu na ujenzi wa viwanda vya kuzalisha barafu.

Maeneo mengine ya mkataba huo ni ujenzi wa viwanda vya vyakula vya samaki, viwanda vya kusarifu dagaa, ujenzi wa kituo cha kufanya utafiti wa uvuvi na mali asili za baharini na ujenzi wa chuo cha kufundishia masuala ya ufugaji wa viumbe maji.

Nae Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Evergreen amesema kampuni yake inamkakati wa kuimarisha uvuvi hapa Zanzibar kwa kutumia vifaa vya kisasa hatua itakayoongeza uzalishaji wa mazao ya baharini na hatimae kuinua uchumi wa wananchi.