Polisi magharibi mwa Kenya wamemkamata mtu anayejiita mhubiri ambaye hivi majuzi alisema alitaka kukutana na Rais William Ruto ili kuwasilisha ujumbe wa kinabii.

Joseph Chenge wa kanisa la Jerusalem Mowar alikamatwa jumatano jioni pamoja na waumini 11 wa kanisa lake katika kijiji cha Ruri kaunti ya Homa Bay.

Afisa upelelezi wa jinai wa Homa Bay, Abed Kavoo alisema wanamshikilia Chenge kwa tuhuma za kuendeleza mafundisho ya kidini ya kutiliwa shaka.

Kavoo amesema uchunguzi wa awali umefichua kuwa kasisi huyo alikuwa akuwazuilia wagonjwa katika kanisa lake kwa kisingizio cha kuwaombea ambapo wagonjwa watano waliokolewa kutoka kanisa la mhubiri huyo.

Polisi wamesema shughuli za kanisa la Chenge zinakiuka sheria kwa vile halijasajiliwa.