Na mwandishi wetu

Mkuu wa mkoa wa kusini unguja Mh: Rashid Hadid Rashi amesema katika kuadhimisha Miaka 59 ya Muungano wa  Tanganyika na Zanzibar Serikali ya Mkoa wa Kusini unguja imeandaa Kongamano kubwa litakaloweza kutoa Elimu kwa Umma kuelewa juu ya tunu ya Muungano.

Akizungumza na Vyombo vya Habari huko Ofisini kwake Tunguu Mkuu huyo amesema hatua hiyo itasaidia Wananchi hususan Vijana kuelewa Historia na Faida ya Kuunganishwa kwa Nchi  hizi mbili  sambamba na kufahamu maendeleo yaliopo katika Muungano huo na kuzitumia ipasavyo Fursa mbali mbali zilizopo ikiwemo za Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii.

Akizungumzia Miaka 59 ya Muungano huo Mh: Rashid amesema ndani ya kipindi hicho Mkoa huo umepata Mafanikio mbali mbali ikiwemo kutekelezwa kwa Miradi Mbalimbali ya kimaendeleo kama vile Majengo ya Kisasa, Miundombinu ya Barabara pamoja na Maji Safi na Salama .

Aidha amesema kwa Mkoa huo Sherehe hizo zimeanza kwa Shuhuli za Usafi katika Maeneo mbali mbali ya Mkoa huo, Dua na Sala pamoja na Mpira wa Miguu ambapo kilele chake kitafanyika Ukumbi wa Dk: Ali Muhammed Shein Tunguu huku akiwataka Wananchi kujitokeza kwa wingi katika Sherehe hizo.

Sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar huadhimishwa kitaifa kila ifikapo Tarehe 26 April ambapo kwa Mwaka huu Sherehe hizo zinafanyika Kimkoa ikiwa ni agizo la Mh: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk; Samia Suluhu Hassan.