Na mwandishi wetu

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Bw. Rajab Yussuf Mkasaba ameitaka Jamii kuacha kuwafanyia vitendo vya Udhalilishaji watoto wenye ulemavu kwa  kuwafungia Ndani  kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki zao za Msingi.

Akifunguwa kongamano la  Wadau wa Maendeleo Jumuishi katika jamii (Cbid) huko Ofisi ya Mkoa Tunguu, Mkasaba amesema kila mmoja ni Mlemavu mtarajiwa hivyo kitendo cha kuwafungia ndani watu wenye Ulemavu ni kosa na halikubaliki katika Jamii kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na haki za binaadamu.

Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Khamis Ussi Debe amesema baraza kwa kushirikiana na Taasisi ya Madrasa Early Childhood wameweza kuwahamasisha watu wenye ulemavu kutetea haki zao, huku wakiwa tayari kuzungumza changamoto zinazo wakabili.

Nao baadhi ya washiriki katika Kongamano hilo wakazungumzia hali ya Watu wanaowatumia watu wenye Ulemavu kuwa omba omba kwa maslahi yao, hivyo wameiomba Serikali kuwachukulia hatua zinazofaa.

Kongamano la  wadau (Cbid) lililoanadaliwa na Taasisi ya Madrasa Early Childhood kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu lenye kauli Mbiu "Hakuna Linalotuhusu Sisi Pasi Na Sisi"  na kuwashirikisha Masheha Wa Wilaya Ya Kusini, wadau wa watu wenye ulemavu kwa lengo la kujadili changamoto na kuzitafutia ufumbuzi.