Na mwandishi wetu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri zote nchini ziendelee kutekeleza agizo la Serikali la kutenga maeneo rafiki yatakayowawezesha vijana kushiriki shughuli za uzalishaji mali ili kuwaepusha na kero ya kufanya biashara kwenye maeneo hatarishi.

Ametoa agizo hilo (Jumatano, Oktoba 12, 2022) alipozindua Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Gymkhana mkoani Kagera. “Maeneo haya ni lazima yawe na sifa zinazoendana na shughuli zinazofanywa na vijana”.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako ashirikiane na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Angela Kairuki ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo.

Mbali na agizo hilo, Mheshimiwa Majaliwa amewaasa vijana kutumia vizuri fursa zilizopo nchini katika kujiletea maendeleo na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, ambayo inayoikabili dunia kwa sasa.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa fursa nyingine kwa vijana ni uhusiano mwema wa kidiplomasia na nchi zote duniani. “Fursa hii ikitumiwa vizuri na kundi la vijana wataweza kunufaika na kusonga mbele kimaendeleo”.

Akizungumzia kuhusu suala la mitaji, Waziri Mkuu amesema kuna  mifuko mingi ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, hivyo waitumie ili kupata mikopo hususan mikopo itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri na kuwekeza katika miradi yenye tija.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewasihi vijana wawe wazalendo na walinzi wa miundombinu ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. “Wakati Serikali inaboresha miundombinu ya kiuchumi, uendelevu wake unategemea sana uzalendo na hali ya kujitegemea kwa Watanzania.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma amesema maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa yanatoa fursa kwa vijana kukutana, kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mbalimbali za uzalishaji mali na uzalendo.

Naye, Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema Wiki ya Vijana kwa mwaka huu imelenga kuhamasisha ushiriki wa vijana katika kuleta maendeleo  endelevu. “Vijana wanapaswa kutafakari kikamilifu ushiriki wao katika ujenzi wa uchumi wa Taifa hasa kipindi hichi  ambacho Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amefungua fursa za kiuchumi na vijana wakiwa wanufaika wakuu.”