AFISI YA RAIS, KAZI, UCHUMI NA
UWEKEZAJI - ZANZIBAR.
TAARIFA KWA UMMA 07/10/2022.
Hivi karibuni kumekuwa na Taarifa zinazosambaa kwenye Vyombo vya
Habari ikiwemo Mitandao ya Kijamii zinazohusiana na kuvunjwa kwa Mkataba wa
Ardhi uliotolewa kwa Kampuni ya Pennyroyal Limited inayoendesha Mradi wa Blue
Amber uliopo Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja. Mradi huu wa Uwekezaji
ulisajiliwa na Mamlaka ya Kukuza na Kulinda Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), chini ya
Sheria ya Mamlaka ya Kukuza na Kulinda Uwekezaji Zanzibar, Sheria Namb. 14,
2018 pamoja na marekebisho yake.
Taarifa hizo pamoja na mambo mengine zinadai kuwa, ufutwaji wa Ardhi
hiyo haukuzingatia Masharti ya Kisheria na kwamba, mwekezaji huyo alipata
Taarifa kuhusu Suala hilo baada ya ombi lake la kuhuisha Kibali cha Ujenzi
kukataliwa na ZIPA. Taarifa hizo hazina ukweli na kwamba, watoaji wa Taarifa
hizo wanalengo la kupotosha umma na kuzorotesha Juhudi za Serikali katika
Uwekezaji.
Serikali imekuwa na uvumilivu mkubwa juu ya Mradi huu hasa ukizingatia
Kasi Ndogo ya Utekelezi wa Mradi huu kwa
kulinganisha na muda tokea ulipoanza. Aidha, Serikali imesamehe takriban Shilingi za Kitanzania milioni 354 za
kodi zilizotokana na uingizwaji wa vifaa mbali mbali vya mradi. Haya yote
yamefanyika kwa ajili ya kuwezesha na kuwepesisha Utekelezaji wa Mradi huu.
Tunapenda umma ufahamu kuwa, uamuzi uliofikiwa na Serikali ya kufutwa
kwa Sehemu ya Ardhi ya Uwekezaji iliyotolewa kwa Kampuni ya Pennyroyal Limited
ilitokana na maamuzi halali ya Mahkama yaliyotolewa kwenye Kesi ya Madai Nambari 05/2013
iliyohusisha sehemu ya Ardhi iliyotolewa kwa mwekezaji huyo. kati ya hekta
411.92 alizopewa mwekezaji tokea mwaka 2015 ni hekta ishirini (20) tu ambazo ni
chini ya asilimia tano (5%) ndizo zilitumika na ndizo zilizoingia katika kadhia
hii na sio eneo lote alilopewa Mwekezaji.
Kufuatia mgogoro uliojitokeza kwa hekta hizo 20, Mahkama iliamuru
hekta hizo apatiwe muhusika aliyewasilisha madai yake katika Mahkama. Hata
hivyo, Mwekezaji huyo aliamua kufanya ujenzi katika eneo la hekta 20 ambalo
lilikuwa na mgogoro kati yake na mdai.
Ni matarajio yetu kuwa Mwekezaji angeheshimu maamuzi ya Mahkama na
kutii sheria kama ilivyofanyika kwa upande wa Serikali.
Aidha, katika hatua za kutekeleza Maamuzi ya
Mahkama, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi ilifuta Mkataba wa Ukodishaji
Ardhi ya Uwekezaji uliyotolewa kwa mradi huo kupitia Barua yenye Kumbukumbu
Nambari CHD.167/173/02/49 ya tarehe 7 Januari 2022, ili kuwezesha Serikali
kupima upya eneo lililobaki na kutoa Mkataba mpya wa Ardhi ya Uwekezaji kwa
Kampuni hiyo.
Hata hivyo, kabla ya utekelezaji wa maamuzi hayo, Serikali kupitia Wizara
ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi iliijuilisha Kampuni ya Pennyroyal
kuhusiana na dhamira ya kutekeleza maamuzi hayo kwa Barua yenye Kumbukumbu
Namba AB.81/167/01/41 ya tarehe 15 Octoba, 2021 hivyo, mwekezaji huyu
alikuwa na Taarifa zote zinazohusiana na
suala hili.
Serikali kwa kutambua umuhimu wa uwekezaji nchini ilichukua juhudi
mbali mbali za kufanya mawasiliano na mwekezaji huyo kwa lengo la kufanya naye
mazungumzo kwa nia ya kutafuta ufumbuzi wa kadhia hiyo. Juhudi hizo za Serikali
zilifanyika ikiwa ni ishara ya kuthamini uwekezaji uliowekezwa na kuonesha kuwa
Serikali iko tayari kutafuta suluhu ya kadhia hiyo.
Pamoja na juhudi hizo za Serikali, bado mwekezaji huyo alikataa
kukutana na Serikali na badala yake kukimbilia kwenye Vyombo vya Habari, jambo
ambalo limetushangaza kwa kuzingatia kuwa mwekezaji huyo anatambua kuwa maamuzi
yaliyotolewa na Serikali yalitokana na Maamuzi ya Mahkama kwa sehemu tu ya eneo
alilopewa kwa uwekezaji na sio ardhi yote.
Hatua iliyofikiwa na mwekezaji huyo imezidisha hofu na mashaka kwa
Serikali dhidi wa uwekezaji wake, hasa kwa kuzingatia kuwa mwekezaji huyo
ameshindwa kufanya uwekezaji kulingana na mpango wake wa biashara
ulioidhinishwa kwa miaka minane (8) sasa tangu Mradi huo uliposajiliwa na ZIPA
licha ya vivutio na fursa za uwezeshaji alizopatiwa na Serikali
katika kuhakikisha kuwa anafanikisha
uwekezaji wake.
Tunapenda kuwatoa wasiwasi wawekezaji wote na kuwahakikishia kuwa,
Zanzibar ni sehemu salama na kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania zinathamini mchango wa wawekezaji.
Aidha, Serikali zote mbili zimeweka kipamumbele katika kuboresha mazingira ya
uwekezaji nchini na kwa hali yoyote ile Serikali haiko tayari kuona juhudi hizo
za Serikali zinazimwa na wawekezaji wachache walioshindwa kutekeleza wajibu
wao. Sambamba na hayo, Serikali daima italinda na kusimamia Uhuru na Maamuzi
halali yanayotolewa na Mahkama pamoja na kuhakikisha maslab hi ya wawekezaji
yanalindwa.
Ahsanteni.
0 Maoni