Wizara  ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, inampango wa kununua vitabu vyote kwa ajili ya kusomea wanafunzi wa Primar na sekondari ili kuondosha changamoto ya upatikanaji wa vitabu pamoja na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.

 

Katibu mkuu wa wizara ya elimu Zanzibar Ali Khamis Juma amesema hayo, katika maadhimisho ya wiki ya maonesho ya vitabu yaliyoandaliwa na Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) yaliyowashirikisha wanafunzi wa Skuli ya Jumbi, halfa iliyofanyika katika ukumbi wa chuo hicho Tunguu  na kusema kuwa mpango huo unatarajiwa kukamilika mwakani.

 

Amesema hivi sasa  mchakato  umeshaanza na wameshafanya mazungumzo na katibu mkuu wa Wizara ya Elimu Tanzania bara ili kuona watoto wao wanasoma kila mtoto na kitabu chake.

 

Katibu Ali amefahamisha kuwa hatua hiyo imekuja kufuatia kikao kilichofanyika na walimu na kueleza changamoto zinazowakabili ikiwemo upungufu wa vitabu ambapo huko nyuma walikuwa wananunua na kuharimu fedha nyingi.

 

Aidha amesema wizara yao imeweka utaratibu mpya wa kuwa na maktaba za nje ya wizara ambapo imeshajenga maktaba moja iliyopo Dunga wilaya ya kati Unguja na timeharimu shilingi milioni 46 hadi kumalizika kwake.

 

Nae, Makamo Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Professa, Mohammed Makame Haji, amesema, serikali kupitia wizara ya elimu imekuwa ikitoa mchango kwa wanaotumia vitabu na wanaosoma vitabu.

 

Mapema Katibu wa Jumuiya ya waandishi wa vitabu Zanzibar, Ali Mwalim Rashid, alisema, jumuiya yao wapo tayari kuwa mstari wa mbele jatika kuhakikisha wanaandika vitabu mbalimbali ili kuona vinasomwa katika skuli mbalimbali na kwenye maktaba zilizopo ndani na nje ya nchi.