Na mwandishi wetu

WAZIRI wa Afya, Ahmed Nassor Mazrui, amesema, jitihada za Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria (PMI) zimechangia kupunguza kasi ya maambukizi ya malaria Zanzibar  kutoka zaidi ya 30% mwaka 2005 hadi kiwango cha sasa cha chini ya 1%.

 Hayo aliyaeleza alipokuwa akizindua mradi mpya wa miaka mitano kuondoa malaria Zanzibar katika Hoteli ya Golden Tulip uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Mkoa wa Mjini Magharib.

 Amesema, mradi huo wa miaka mitano utaondoa kabisa malaria Zanzibar kutoka  1% hadi asilimia 0%  na kuudhibiti ugonjwa huo na kuwa ukanda huru.

 Amesema, katika kipindi cha miaka 16, Wizara ya Afya Zanzibar imenufaika na msaada wa PMI katika safari ya kutokomeza malaria nchini.

 Amesema, PMI kupitia USAID na CDC wamekuwa wakisaidia hatua zilizothibitishwa za kutokomeza malaria kama vile utambuzi na matibabu ya malaria, udhibiti jumuishi wa vimelea vya malaria,  ufuatiliaji na tathmini juu ya ugonjwa huo.

 Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, PMI kupitia Shirika la Okoa Maisha Dhibiti Malaria (OMDM), ilichangia zaidi ya dola milioni 19.3 kwa Serikali ya Tanzania kusaidia juhudi za kutokomeza malaria kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

 Waziri Mazrui, alisema, kupitia OMDM, kumekuwa na baadhi ya maboresho mapambano dhidi ya malaria ikiwemo ufuatiliaji na tathmini ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa kiwango cha uchunguzi wa kesi, kuweka mikakati ya kuondoa hatari ya malaria Zanzibar, kuunganishwa kwa mfumo wa taarifa za kesi za malaria na DHIS2, na uimarishaji wa ufuatiliaji wa vimelea.

 Hivyo, ameelezea matumaini yake kuwa mradi mpya wa PMI TMCM ni muendelezo wa juhudi za kusaidia kutokomeza malaria Zanzibar.

 Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afya  USAID, Anna Hoffman, amesema, kupitia ushirikiano wa karibu na wananchi, taasisi na Serikali ya Zanzibar, Serikali ya Marekani imejitolea kufuata kiwango sawa cha ushirikiano na ZAMEP na asasi za kiraia kusonga mbele kuimarisha mifumo ya afya ili kuimarisha na kuongeza juhudi za Tanzania katika kukomesha hali hiyo.

 Alisema, USAID inajivunia kuwa sehemu ya mafanikio haya ya ajabu, lengo la pamoja ni kukomesha malaria.

 Alisema, kupitia OMDM, viwango vya uchunguzi wa kesi za malaria viliongezeka kutoka chini ya 50% mwaka 2018 hadi zaidi ya 95% mwaka 2022, ikiwa na maana kwamba watu wengi zaidi wanapimwa na kutibiwa malaria na kulindwa dhidi ya maambukizi ya baadaye, hatua muhimu zinazotusogeza karibu na kufikia kutokomeza malaria.