Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akizungumza katika kikao cha makabidhiano ya Ofisi kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax kilichofanyika Mtumba jijini Dodoma.

 Na Mwandishi wetu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amewataka watumishi wa Wizara kuendelea kuchapa kazi kwa bidii, ufanisi na kushirikiana ili kufikia matarajio ya serikali na wananchi kwa ujumla.

 Dkt. Tax ametoa rai hiyo katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma mara baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.

 Dkt. Tax amesema watumishi wa Wizara wanatakiwa kuhakikisha wanatumia weledi na kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu ya Wizara ili kuleta tija na ufanisi wakati wote.

Ameongeza kuwa kazi ya kukuza uhusiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali, Jumuiya za kikanda na kimataifa haiwezi kufanikiwa ikiwa watumishi hawatashirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kama timu huku wakizingatia weledi, uzalendo na ubunifu kwa maslahi mapana ya taifa.

 Akizungumza katika makabidhiano hayo, Balozi Liberata Mulamula amewashukuru Watumishi wa Wizara kwa ushirikiano waliompatia alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambao ulimuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

 Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Sokoine alisema Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kumuahidi Dkt. Tax kuwa watumishi wako imara na wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni na hivyo kuleta tija kwa wizara na taifa kwa ujumla.