Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akizungumza na wajumbe wa Baraza la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (hawapo pichani) wakati akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa Baraza kwa wajumbe wa Baraza jipya wa Ofisi hiyo yaliyofanyika jijini Dodoma.

 

Na Mwandishi Wetu

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) kutumia mafunzo wanayopatiwa kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa Baraza la wafanyakazi katika kuweka mahala pa kazi kuwa sehemu salama katika utendaji wa kazi na kuhakikisha kuwa wajumbe wa OWMS wanatekeleza majukumu waliyokasimiwa.

Dkt. Luhende ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wajumbe wapya wa Baraza la Wafanyakazi wa OWMS yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Takwimu jijini Dodoma ambapo amesema kuwa mada tatu zitawasilishwa kwa wajumbe hao ikiwemo Wajibu na Majukumu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi; Kupitia Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi; na Umuhimu wa Baraza la wafanyakazi mahala pa kazi.

Amewataka wajumbe kutumia fursa hiyo kuzijua hadidu za rejea ambazo zitawaongoza katika utendaji kazi wa kila siku na kutekeleza majukumu katika kipindi chote cha miaka mitatu watakachokuwa wajumbe wa Baraza hilo  kuwa nguzo kati ya Baraza na watumishi wengine kwa kuwa Baraza la wafanyakazi ni chombo muhimu mahala pa kazi na kuwa sehemu salama ili kuleta tija katika utendaji kazi wa kila siku wa OWMS na amewataka wajiandae kuhamia Dodoma mwaka huu.

Akitoa mada ya Umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma, Samuel Nyungwa amesema kuwa ni muhimu kwa kila mtumishi kujiunga na chama cha wafanyakazi kwa sababu ni taasisi pekee ya wafanyakazi ambayo imeundwa kwa ajili ya kulinda na kutetea haki kwa kuweka sawa mahusiano ya kazi kati mfanyakazi na mwajiri wake mahali pa kazi.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sebastian Innosh amewasilisha mada kuhusu umuhimu na uendeshaji wenye tija wa mabaraza la wafanyakazi ambapo amesema kuwa mabaraza yanatakiwa kushauri na kujadili masuala muhimu ya taasisi; kutumia rasilimali watu na fedha kwa manufaa na uendelevu wa taasisi husika na taifa kwa ujumla; na kuimarisha mahusiano mema na kudumisha amani na utulivu mahala pa kazi.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemarila Rutatina amesema kuwa mkataba wa Baraza la Wafanyakazi unaleta mafanikio na ushirikiano mahala pa kazi kwa kuwa unawaweka pamoja na kuwaleta karibu watumishi mahali pa kazi.