Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Sumbawanga Rainer Lukala wakati akiongea na wanufaike wa mikopo katika vijiji vya Msila na Ilemba ikiwa ni ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Na mwandishi

 Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga imepongezwa kwa kuwezesha walemavu na wanawake kupata mikopo inayotokana na mapato ya ndani hatua inayosaidia kukuza uchumi wa kaya.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Sumbawanga Rainer Lukala wakati akiongea na wanufaike wa mikopo katika vijiji vya Msila na Ilemba ikiwa ni ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Maelekezo ya Ilani ya CCM ni kutumia fedha asilimia kumi ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kuwezesha mikopo kwa makundi ya wanawake, vijana na walemavu kwa riba nafuu. Tunawapongeza halmashauri kwa kufanikisha hilo” alisema Lukala.

Halmashauri hiyo katika mwaka 2021/22 imetoa mikopo ya shilingi Milioni Sita (6) kwa kikundi cha wanawake wa kijiji cha Msila na shilingi Milioni Tano (5) kwa walemavu wawili wa kijiji cha Ilemba.

Lukala alitoa wito kwa wanufaike wa mikopo hiyo kuwa na utaratibu wa kuutunza fedha kwenye akaunti za benki ili wawe na uhakika wa kufanya marejesho na kuwa halmashauri itoe kipaumbele kwa vikundi vinavyorejesha vizuri ili wapate mikopo awamu ya pili.

Naye Katibu wa Kikundi cha Kilimo Kwanza kijiji cha Msila kata ya Mfinga Anastazia Joseph alisema anaomba halmashauri iongeze kipindi cha kurejesha mkopo toka mwaka mmoja hadi miwili kwa kuwa rejesho la shilingi 500,000 kila mwezi kati ya mkopo wa shilingi Milioni 6 ni kubwa.

Kikundi hicho chenye wanachama kumi na mbili (12) kinajishughulisha na kazi za kilimo ambapo wamelima hekari nne za mahindi na moja ya alizeti huku wanachama wakiweka akiba na kukopeshana.

Kwa upande wake Joseph Mwendapole mnufaika wa mikopo ya walemavu toka kijiji cha Ilemba alisema ameweza kununua pikipiki kutokana na mkopo wa Milioni 2.5 hatua inayomwezesha kupata kipato cha kuutunza familia na shughuli za kilimo.

Mnufaika huyo aliwaambia wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Rukwa kuwa kwa sasa anamiliki pia bajaji kutokana na mkopo aliopata awali ambapo ametoa wito kwa halmashauri kuwapa pia wahitaji wengine mikopo ikiwemo vijana kwa masharti nafuu.

“Ninaahidi nitajitahidi kufanya marejesho ili walemavu wengine wapate mikopo hii. Sasa napambania uzee wangu ili niwe na amani uzeeni kwa kuwa na uhakika wa kipato” alisema Mwendapole.