Rais wa Zanzibar na
mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al-Haji Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka
waumini wa Dini ya Kislamu kutumia maadhimisho ya Mazazi ya Mtume Muhamad
(S.A.W) kwa kudumisha Amani na mshikamano katika jamii.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo wakati
akimuwakilisha Rais Dk. Mwinyi katika sherehe za Maulid ya Kusifu Mtume
S.A.W yalioandaliwa na waumini wa Tumbatu Jongowe Mkoa wa Kasakazini Unguja.
Alisema kuwa, moja
kati ya Sifa za Mtume Muhamad S.A.W alikuwa ni kiongozi mwenye sifa ya
kuwaunganisha na kuwaleta pamoja watu kwa kutumia maelekezo ya Dini ya kislamu
bila ya kujali tofauti zao.
Mhe. Alifafanua kuwa
kuna kila sababu kwa waumini na wananchi wa Tumbatu Jongoe na maeneo mengine
kuiga kigezo chema kutoka kwa kiongozi wa Umaa wa Kisalamu kwa kudumisha Umoja,
upendo na mshikamano bila ya kujali tofauti zozote walizonazo ikiwemo
tofauti za kisiasa.
Aidha, aliwahakikishia
wananchi wa Tumbatu Kuwa, serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk.
Mwinyi itahakikisha shughuli za wananchi zinaendelea vyema kwa kuwafikishia
huduma za msingi ikiwemo masuala ya kimaendeleo.
Pamoja na mambo
mengine Makamu wa Pili wa Rais aliwakumbusha waumini hao kuendelea kumuombea
Dua Rais Dk. Mwinyi ili Mwenyezi Mungu amewezesha kuyatekeleza yale yote
aliyoyaahidi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Kabla ya Kumkaribisha
Mgeni rasmi Naibu Mufti Mkuu Sheikh Mahamoud Mussa Wadi aliwakumbusha waumini
hao kushikamana na muongozo wa Dini ya kisalamu unaowataka waislamu kuishi
pamoja na kuachana na tofauti ili kupata radhi za Allah (S.W).
Nae, Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed Mahamoud aliwataka wananchi wa Tumbatu na
Zanzibar kwa Ujumla kuzitumia sherehe za Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume
(S.A.W) kwa kuwaunganisha wananchi wote kuwa kitu kimoja.
Mamia ya waumini kutoka Tumbatu Jongowe walishirikiana pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika sherehe ya Maulid ya Mtume Muhamad (S.A.W) yaliofanyika kijijini humo.




0 Maoni