Na Mwandishi wetu
Chama cha Waandishi wa Wahabari Wanawake Tanzania, Zanzibar, (TAMWA ZNZ) kinawapongeza Bi Salma Ali Hassan Khamis na Bi Mwanamkaa Abdulrahman Mohammed kwa kuteuliwa kuiongoza Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar.
Afisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka Zanzibar ina majukumu mengi
yakiwemo ya kupokea na kukagua faili
zote zinazotoka polisi, kuchambua ushahidi wa upelelezi uliotoka polisi, kupeleka
faili za kesi mahakamani, kuendesha kesi Mahakamani kwa kuuwakilisha upande wa
Serikali na kukata rufaa iwapo haitaridhika na maamuzi ya Mahakama kuhusiana na
shauri lolote
Kupitia uteuzi huo
uiliofanywa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar,Dkt
Hussein Ali Mwinyi hivi karibuni, Bi Salma Ali Hassan Khamis
ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Afisi hiyo na Bi Mwanamkaa
Abdulrahman Mohammed kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka katika Afisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar.
Hawa ni viongozi wa
kwanza wanawake kuongoza Afisi hiyo katika nafasi hizo kuu kabisa na hivyo
kuongeza uwepo wa wanawake katika nafasi za uongozi kwa jumla, hali ambayo
inahimizwa kwa maendeleo ya mwanamke na nchi kwa jumla.
TAMWA - ZNZ inaamini
kuwa kuwepo kwa viongozi hao, kesi za udhalilishaji na ukatili wa wanawake na
watoto zitapata msukumo mpya katika ufuatiliaji na uchunguzi na kwa muda mfupi
ili kukomesha kabisa vitendo hivyo vilivyokithiri nchini na ambavyo
vinawaathiri zaidi wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa takwimu
kutoka Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, jumla ya kesi 838 za udhalilishaji ziliripotiwa kuanzia
mwezi wa Januari hadi Agosti, 2021 ambapo wanawake walioathirika ni 679 sawa na
asilimia 81 na wanaume ni 166 sawa na asilimia
19.8.
Ukatili mwingine ni
wanawake na watoto kupigwa kwa mapanga kutokana na sababu zisizokuwa za msingi
na kwamba wengi wa wahalifu bado hawajakamatwa. Hivyo, tunashauri Wakurugenzi wa Mashtaka kuandaa utaratibu
maalum wa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kurahisisha uchunguzi katika
matukio ya aina hii.
TAMWA - ZNZ inawatakia
kila la kheri Wakurugenzi hao katika
majukumu yao mapya na muhimu na Mwenyezi Mungu awaongeze hekima, busara,
ushirikishaji na uadilifu zaidi.




0 Maoni