RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiondoa kipazia na Mwakilishi wa Shirika
la Umoja wa Mataifa linalishughulika na Masuala ya Jinsia na Uwezeshaji wa
Wanawake (UN WOMEN) Bi.Hodan Addou, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya “HeforShe”
uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar na (kulia
kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Marian Mwinyi na Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar Mhe.Nassor Ahmed Mazrui na
(kushoto) Mwakilishi Mkaazi wa UN Nchini Tanzania.Bw.Zlatan Millisic. Na mwandishi wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi ametunukiwa cheo cha heshima na
jukumu la kuwa kinara au bingwa wa Taifa wa Kampeini ya “The National Champion
for the UN Women HeForShe campaign” na kuahidi kwamba atakitumikia vyema cheo
hicho.
Ahadi hiyo ameitoa leo wakati akisoma hotuba yake ya uzinduzi wa Kampeni ya
HeForShe iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la UN Women, ambalo ndilo
lililomkabidhi Rais cheo hicho katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Hoteli ya
Verde, Zanzibar.
Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi aliahidi kwamba atakuwa bega kwa bega
katika kupigania na kuimarisha usawa, haki, maslahi na ustawi wa wanawake
pamoja na usawa wa aina zote kwa jinsia zote.
Alisema kuwa amekuwa akijitahidi kwa nguvu na uwezo wake wote kutoa haki
kwa misingi ya usawa kwa jinsia zote kwani yeye ni muumini wa kweli wa haki na
maendeleo ya wanawake.
“Suala la kuwatumia wananchi wa Zanzibar wa jinsia zote kwa misingi ya haki
na usawa ni utii wa Katiba ya Zanzibar ambayo nimeilia kiapo kwamba, nitaitii
kwa hivyo suala hilo kwangu ni la lazima”,alisema Rais Dk. Mwinyi.
Aidha, alisema kwamba suala la kuwepo kwa usawa wa kijinsia na kuimarisha
maendeleo ya wanawake ni la lazima hasa ikizingatiwa kwamba Sensa ya Watu na
Makaazi iliyofanywa mwaka 2012 ilionesha kwamba idadi ya wanawake Zanzibar ni
672,892 na wanaume 630,677 hivyo, ni dhahiri kwamba maendeleo hayawezi
kupatikana iwapo sehemu kubwa ya nguvu kazi ya Zanzibar itawachwa nyuma na bila
ya kuwezeshwa kwa misingi ya usawa.
Rais Dk. Miwnyi alisema kuwa hivi sasa amekuwa akiyatekeleza kivitendo yale
aliyoyalia kiapo na yale aliyoyaahidi kwa nyakati mbali mbali katika teuzi
anazozifanya ambapo amekuwa akiteua viongozi bila ya ubaguzi wa aina yoyote
kwani amekuwa akijali sifa na uwezo wa watu.
Aliongeza kuwa amekuwa akiteua wanawake katika nafasi mbali mbali na kuwashirikisha
kikamilifu katika utoaji wa maamuzi katika masuala muhimu ya Serikali na nchi
kwa jumla huku akisisitiza kwamba
maendeleo yaliyopatikana hapa Zanzibar na katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika kuimarisha usawa wa kijinsia ni ya kupigiwa mfano.
Rais Dk. Miwnyi alisema kuwa idadi ya viongozi wanawake hapa Zanzibar
inaendelea kupanda ikilinganishwa na miaka ya nyuma vile vile, ameteua Katibu
wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi mwanamke na kumteua Mwanamama
kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), ikiwa ni mara ya kwanza kwa nafasi
hizo kushika wanawake.
Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza wanawake aliowateua
katika Serikali yake kwani hawajamuangusha na wanafanya kazi vizuri na vyema
kuliko wanaume na kueleza kwamba takwimu zilizopo za uongozi kati ya wanawake
na wanaume Serikali zinaweza kubadilika muda si mrefu.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwataka Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Job Ndugai na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali
Maulid kushirikiana na UN Women kwa kwenda kufikisha ujumbe maalum katika vyombo vya kutunga sheria
wanavyoviongoza kuhusiana na malengo na maudhui ya Kampeni hiyo.
Rais Dk. Mwinyi aliiagiza Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jisnia na
Watoto Zanzibar pamoja na taasisi zote za Serikali kufanya kazi kwa karibu na
Shirika la UN katika kutekeleza malengo na maazimio ya Kampeni hiyo ili kuzidi
kuimarisha uwasa wa kijinsia na maendeleo ya wanawake hapa Zanzibar.
Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea
kushirikiana na Shirika la UN Women katika kupambana na vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia, unyanyasaji, mimba za umri mdogo, utelekezaji wa
watoto na mambo yote ambayo ni kikwazo kwa maendeleo ya wanawake na watoto.
Nae Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar Nassor
Ahmed Mazrui alieleza hatua zinazochukuliwa na Wizara yake katika kuhakikisha
inapambana vyema na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Nao Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai na Spika
wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid walimuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba
wanamsaidia kufikisha Kampeni hiyo na kuwa tayari kwa marekebisho yoyote ya
sheria ambayo bado ni kikwazo kwa maendeleo ya Kampeni hiyo.
Viongozi wa UN hapa nchini kwa upande wao na baadhi ya Mabalozi wa nchi za
Ulaya waliohudhuria mkutano huo katika hotuba zao waliahidi kuendelea kuiunga
mkono Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kampeni hio na kumpongeza Rais Dk.
Mwinyi kwa jinsi anavyojali suala zima la jinsia katika uongozi wake huku
wakiiwapongeza wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekekeleza kwa
vitendo suala hilo na kuwa kinara kwa kuwa na Rais mwanamama.
BAADHI ya Mawairi wakifuatilia hutuba ya Rais wa
Zanbzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi,
wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Kampeni ya “HeforShe” iliozinduliwa katika
ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa
Kampeni ya “HeforShe” iliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Jijini
Zanzibar leo 4-11-2021
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Bw.Zlatan Millisic, wakiwa katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Kampeni ya “HeforShe
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakisalimia na
Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa Nchini Tanzania Bw. Zlatan Millisic na
Mwakilishi wa Shirika la UN linaloshughulika na Masuala ya Jinsia na Uwezeshaji
wa Wanawake (UN WOMEN) Bi. Hodan Addou, walipowasili katika viwanja vya Hoteli
ya Verde Mtoni kwa ajili ya Uzinduzi wa Kampeni ya “HeforShe”
0 Maoni