Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia kwenye ufunguzi wa Kongamano la Kumbukizi ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad lililofanyika leo tarehe 05 Novemba, 2021 katika ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar.
 Na mwandishi wetu

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema njia ya kuendelea kumuenzi Maalim Seifu Sharif Hamad ni kudumisha Utamaduni wa Siasa za Majadiliano hatua ambayo itachangia kuleta maendeleo endelevu Zanzibar na Taifa kwa ujumla.

Rais Samia ameyasema hayo akihutubia kwenye ufunguzi wa Kongamano la Kumbukizi ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad lililofanyika leo tarehe 05 Novemba, 2021 katika ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar.

Raisi Samia amesema Maalim alikuwa ni Makutano ya watu, amekuwa kiongozi wa watu na alieishi na watu na watu ikatokea kumshiba katika mioyo yao

"Tunakutana hapa kwa ajili yakumbukumbu ya Maalim Seif, hata katika uhai wake yeye alikuwa ni makutano ya watu, tuliomfahamu kwa miaka mingi tumemjua Maalim Seif kama mtu wa kukutanisha watu daima alikuwa na watu nyuma yake, alikuwa kiongozi wa watu anayeishi na watu, aliyetokana na watu na watu wakamshiba katika mioyo yao,"- Rais Samia

"Watu kukusanyika hapa leo baada ya kifo chake si jambo la kushangaza hata kidogo, uimara wake, utu wake, fikra zake na uthabiti wa kauli zake na utajiri wa moyo wake ni kati ya mambo mengi yaliyofanya watu kumpenda, kumtumaini na kumheshimu,"- Rais Samia

"Pamoja na kwamba Maalim alifanya kazi ya Ualimu na akaitwa Maalim Seif lakini alikuwa Mwalimu wa watu sio tu wa wanafunzi darasani, hata ukimvua vyeo vyote alivyowahi kushika bado anabaki kuwa Maalim wa watu, naipongeza Taasisi ya Maalim Seif kwa kuandaa Kongamano hili kumuenzi"- Rais Samia

Maalim Seif Sharif Hamadi amewahi kushika nafasi tofauti kipindi cha uhai wake ikiwemo Waziri kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mkuu wa Chama kilichokua cha upinzani Zanzibar kwa miaka hiyo CUF na hadi umauti unamkuta  alikua Makamo wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume walipokutana kwenye ufunguzi wa Kongamano la Kumbukizi ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad lililofanyika leo tarehe 05 Novemba, 2021 katika ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza jambo na Bi Awena Sinani Masoud aliyekua mke wa Hayati Maalim Seif Sharif Hamad baada ya kufungua Kongamano la Kumbukizi ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad lililofanyika leo tarehe 05 Novemba, 2021 katika ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar.