Na mwandishi wetu

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi   amesema Maalim Seif Sharif Hamadi atakumbukwa kwa mengi mazuri aliyoyafanya nchini ikiwemo kuhakikisha Amani, Mshikamano na Upendo unaimarika na kudumu.

Amesema Maalim Seif Sharif Hamadi alikua  mwana maridhiano wa kweli na kielelezo halisi ni juhudi zake katika kuhakikisha Nchi inakua na amani baada ya uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Dr Mwinyi amezitoa taarifa hizo hii leo katika Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad, katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, iliyopo Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo mgeni rasmi ya hafla hiyo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

“Mimi binafsi, nimebahatika kufanya kazi kwa karibu sana na hayati Maalim Seif Sharif Hamad akiwa ni Makamu wangu wa Kwanza wa Rais katika hii Awamu ya Nane ya Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa”.

“Bahati mbaya sana kutokana na kudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu hatukubahatika kuwa nae kwa kipindi kirefu sana ndani ya uongozi wa Serikali hii na Mwenyezi Mungu kumpenda zaidi na kumchukua, hakika pengo lake haliwezi kuzibika ndani ya Serikali na katika Jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla”,alisema Rais Dk. Mwinyi.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Maalim Seif hakuwa ni mtu mwenye kujikweza, kiburi au majivuno daima alikuwa ni mtu alieweka maslahi ya Zanzibar kwanza na hakuwa mbinafsi wala mchoyo katika kushauri au kutoa hekima na nasaha zake kwa viongozi vijana wao.

Aliongeza kuwa katika kipindi alichofanya kazi nae aliweza kuvuna na kujifunza kwake mambo mengi yenye lengo la kufunza na kuthamini mshikamano, maelewano na maendeleo ya nchi kwa jumla.