Uzinduzi huo wa mbio hizo ulifanyika leo (Novemba 06. 2021) mapema saa 12
za asububi kwa kuanza kutimua vumbi katika eneo la “Mapinduzi Square” Mwembe
Kisonge Jijini Zanzibar na kuishia katika uwanja wa Amaan kwa kupitia katika
mzunguko wa maeneo mbalimbali yaliyopangwa ambapo wanariadha hao walianza mbio
hizo wakiwemo wakimbiaji wa kilomita 10
na wale wa kilomita 21.
Mara baada ya uzinduzi huo Rais Dk. Mwinyi akiwa na Mama Maria Mwinyi
aliwaongoza viongozi akiwemo Makamo wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla , wananchi pamoja na vikundi
mbali mbali vya mazoezi katika matembezi ya kilomita nne yaliyoanza hapo “Mapinduzi Square” Mwembe
Kisonge hadi uwanja wa Amaan, Jijini Zanzibar.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa vyeti kwa baadhi ya wadhamini wa mashindano
hayo kwa niaba ya wenzao pamoja na kutoa kuwavisha nishani washindi wa
mashindano hayo ambapo pia, alipata fursa ya kuangalia mashindano ya riadha ya
wazee kuanzia miaka 60 pamoja na mashindano ya riadha kwa watu wenye ulemavu wa
miguu.
Akitoa maelezo mafupi juu ya mashindano hayo, Mwenyekiti wa “Zanzibar Blue
economy half Marathon 2021” Abdalla Idrissa Majura alieleza kwamba mashindano
hayo ni kwa ajili ya kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kutimiza mwaka mmoja tokea
aingie madarakani kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi.
Majura alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kuonekana kwamba Rais Dk.
Mwinyi ameanza kutekeleza ahadi zake kwa vitendo akiwa na lengo la kuiletea
maendeleo Zanzibar ambapo na wao wakiwa wanamichezo wanamuunga mkono Rais Dk.
Mwinyi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya (CCM).
Aidha, Mwenyekiti huyo alisema kuwa mashindano hayo pia, yanawasaidia
wananchi wa Wazanzibari katika kufanya mazoezi kwa lengo la kupambana na
maradhi yasioambukiza.
Mwenyekiti huyo aliitaja mikakati waliyoiweka katika maandalizi ya
mashindano hayo pamoja na namna ya upatikanaji wa fedha za mashindano hayo
ulivyofanyika na kusisitiza haja ya mashindano hayo hapo mwakani kuungwa mkono
zaidi na Serikali ili yawe ya Kimataifa kama yalivyo mashindano mengine
yakiwemo yale ya Kilimanjaro Marathon.
Alieleza jinsi wadhamini mbali mbali waliojitokeza kuunga mkono mashindano
hayo ya riadha ambapo miongoni mwa wafadhili hao ni Benki ya “National Microfinance Bank” (NMB)
waliodhamini mashindano ya kilomita 21 ambapo mshindi wa mwanzo alikabidhiwa
TZS milioni moja, mshindi wa pili laki 8 na wa tatu laki 5.
Pamoja na hayo, kwa upande wa mashindano ya killomita 10, kwa maelezo ya
Mwenyekiti huyio Benki ya “Kenya Commercial Bank” (KBC) iliyadhamini ambapo
mshindi wa kwanza alipata TZS laki 8, mshindi wa pili laki 5 na wa tatu alipata
laki 3.
Pia, (KCB) wamedhamini mbio fupi za uwanjani ambapo wanariadha wastaafu
kila mmoja atapata TZS laki 1000,000 kwa wanaume na wanawake huku wanariadha
wote 200 watakaoshiriki watapa TZS 50,000 bila ya kujali mshindi wa mwanzo au
wa mwisho.
Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo alisisitiza lengo la Kamati ya mashindano
hayo la kusaidia ujenzi wa soko la Fumba.
Wadhamini wengine wa waliosaidia mashindano hayo ni Benki ya Watu wa
Zanzibar (PBZ), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mohamed Raza kupitia ZAT,
TRA, BUMACO POSTA,World of Sports Kikwajuni, PSSSF Zanzibar, Azam Media,TTCL,
Shirika la Bandari Zanzibar pamoja na Sea Cliff Zanzibar.




0 Maoni