Na mwandishi wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi
ameupongeza utayari wa Jamhuri ya Ireland nchini Tanzania kwa kuahidi
kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi
katika kuimarisha sekta zake za maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo
na Balozi wa Jamhuri ya Ireland nchini Tanzania Bi Mary O’Neil aliyefika Ikulu
kwa ajili ya kujitambulisha.
Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo kwamba Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo
kati ya pande mbili hizo, na kuupongeza utayari wa Jamhuri ya Ireland kuahidi
kusaidia miradi mbali mbali ya maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua za Jamhuri ya Ireland ya kuahidi
kuwawezesha wanawake kutasaidia kwa kiasi kikubwa hasa kwa upande wa wanawake
wanaojishughulisha na shughuli za kimaendeleo wakiwemo wakulima wa mwani ambao
kwa upande wao wamekuwa na changamoto ya kukosa soko la bidhaa yao hiyo.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza hatua ya nchi hiyo kutoa nafasi za
masomo nchini humo na kusisitiza haja ya kuendeleza na kuongezwa zaidi hatua
hiyo ili Wazanzibari walio wengi waweze kupata nafasi za masomo mbali mbali
nchini humo.
Aliongeza kuwa katika eneo la utalii, ambapo Balozi O’Neil aliahidi kwa
nchi yake kwamba atahakikisha anakuwa balozi wa kuitangaza na kuutangaza utalii
wa Zanzibar nchini mwake, alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa
kwani hivi sasa wawekezaji katika sekta hiyo wamekuwa wakija Zanzibar na
kuekeza kwa kasi sambamba na kuongezeka kwa watalii kufuatia kupungua kwa janga
la UVIKO 19 duniani.
Alieleza kuwa suala zima la uhifadhi wa mazingira hasa katika bahari nalo
limepewa kipaumbele zaidi na Serikali ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati
madhubuti ya kuzuia uharibifu wa mazingira huku akieleza kwamba licha ya kuwepo
kwa mabadiliko ya tabianchi na athari zake lakini bado hatua za makusudi
zimekuwa zikichukuliwa kuzibiti hali hiyo.
Kwa upande wa Uchumi wa Buluu, Rais Dk. Miwnyi alimueleza Balozi huyo hatua
na mikakati iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Nane huku akieleza kwamba
Jamhuri ya Ireland inasababu kadhaa za kuunga mkono hatua hizo hasa
ikizingatiwa kwamba nchi hiyo imeweza kupiga hatua kupitia Dira hiyo.
Nae Balozi Bi Mary O’Neil alimueleza
Rais Dk. Mwinyi azma ya Jamhuri ya Ireland ya kuiunga mkono Zanzibar katika
kuendeleza sekta mbali mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono hatua
za kuwawezesha wanawake, nafasi za masomo, mazingira ya upatikanaji wa haki kwa
jamii, sekta ya utalii, mabadiliko ya
tabia nchi, uchumi wa buluu na sekta nyenginezo.
Balozi O’Neil
alieleza jinsi Jamhuri ya Ireland ilivyokuwa na nafasi nzuri ya kuuunga mkono
Uchumi wa Buluu ambao ndio Dira ya Uchumi wa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya
uongozi wa Rais Dk. Mwinyi hiyo ni kutokana na nchi hiyo kuwa na mazingira
yanayofanana na Zanzibar sambamba na kuitekeleza kwa vitendo Dira hiyo nchini humo




0 Maoni