Na mwandishi wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake unaokuja serikali ina jumla ya shilingi bilioni 460 ambazo zitaingizwa katika uchumi wa Zanzibar.    

 Dk. Hussein alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi moja moja na wananchi kupitia vyombo vya habari katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa ndege ikiwa ni maadhimisho ya mwaka mmoja wa uongozi wake.

 Alisema fedha hizo ni pamoja na mkopo wa IMF wa dola za kimarekani milioni 100 sawa na bilioni 230 ambazo ni mgao uliotoka katika serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na mkopo uliokopwa na serikali ya Zanzibar wa shilingi bilioni 230. 

  Aidha alisema lengo la kuingiza fedha hizo katika uchumi wa Zanzibar ni kuhakikisha kipindi cha mwaka mmoja unaokuja ni kuona ahadi zote zilizoahidiwa kwa wananchi ziweze kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa kuliko mwaka mmoja uliotangulia.

 Rais Mwinyi, alisema hatakuwa na muhali kwa kiongozi yoyote atakaechukua theluthi ya fedha hiyo kwa ajili ya maslahi yake binafsi.

 “Bilioni 460 ni fedha nyingi hivi tukikosa uadilifu fedha nyingi zitaingia kwenye mifuko ya watu hivyo natoa idhari hata fedha moja isipotee sitasita kumfukuza mtu na kumpeleka mahakaani,” alisema.

 Dk. Mwinyi akizungumzia fedha za IMF alisema fedha zake zitaingizwa katika sekta maalum zilizoathirika na ugonjwa wa Uviko 19 ikiwemo sekta ya afya, elimu, maji, umeme na kuwawezesha wajasiriamali.

 Kwa upande wa fedha za serikali za shilingi bilioni 230 zilizokopwa Rais Mwinyi alisema zitaelekezwa katika maeneo matatu makubwa ikiwemo kulipa madeni ya wazabuni wanaodai serikali, watu wanaostahili kulipwa fidia ambazo hawajalipwa na madeni ya wafanyakazi wanaoidai wa serikali, barabara za ndani na kutoa fedha hizo kwa ajili ya kuchangamsha uchumi kwa kuingiza fedha hizo katika mzunhuko ili shughuli ziendelee kama ilivyokuwa kabla ya ugonjwa wa korona.

 SEKTA YA AFYA

 Dk. Mwinyi alisema ili kuweza kuimarisha vyema sekta ya afya jumla ya shilingi bilioni 69 kwa ajili ya kuimarisha miradi ya miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali mpya ya ngazi ya Mkoa katika mkoa wa Mjini Magharibi katika eneo la Lumumba ambao ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 14.

 Alisema hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 200 kwa wakati mmoja na itakuwa ya horofa tano na kuwekwa vifaa tiba vya kisasa ikiwemo Seat Scan, IMR, huduma za uchunguzi za maaba za kisasa na huduma za afya za dharura.

  Dk. Mwinyi alibainisha kwamba hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kutoa huduma mbalimbali za kibingwa pamoja na huduma za macho na meno, wodi na kilnik za wagonjwa mbalimbali kwa nia ya kuongeza wigo wa kutoa huduma bora na kupunguza idadi ya watu wanaokwenda hospitali ya Mzanzimmoja ambayo nayo itaendelea kuboreshwa kupitia msaada wa jumuiya ya Benki za kiarabu Badea ili ikidhi hadhi yake ya kuwa hospitali ya rufaa.    

 Sambamba na hilo, Rais Mwinyi, alisema serikali imeamua kutumia fedha hizo za IMF kuboresha na kuipatia vifaa vya kisasa na madaktari wataalamu wa kutosha hospitali ya Abdalla Mzee kisiwani Pemba na kuipandisha hadhi kuwa spitali ya mkoa ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi wa mkoa wa kusini na kisiwa cha Pemba kwa ujumla.

  Hata hivyo alisema pamoja na ujenzi huo serikali itajenga hospitali za wilaya 10 katika ngazi ya wilaya ambayo kila moja itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 100 kwa wakati mmoja pamoja na ujenzi wa nyumba za wafanyakazi zitakazotosha kuhudumia familia 16 kwa gharama ya shilingi bilioni 22.

 “Kwa mara ya kwanza Zanzibar tutakuwa na hospitali mbili za mikoa hospitali 10 katika kila wilaya zote za Unguja na Pemba isipokuwa wilaya ya Mkoani pekee na tayari michoro ya hospitali zote imeshakamilika na taratibu za manunuzi ili kuwapata wakandarasi zitatangazwa rasmi ambapo kazi ya ujenzi itaanza rasmi kabla ya mwezi wa Disemba mwaka huu,” alisema.

 Alisema hospitali hizo zitatoa huduma za uchunguzi kwa kutumia vifaa vya kisasa Digital XRAY Utrasoud, maabara za kisasa, ICU na wodi maalum kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu, magonjwa ya wanawake, upimaji wa mimba, uzazi wa kawaida na huduma za upasuaji.

 Alisema pia serikali itanunua gari 12 za kubebea wagonjwa ambayo kila moja itawekwa katika hospitali ya wilaya pamoja na hospitali mbili za mikoa huku gari tano kwa ajili ya kusambazia dawa katika hospitali na vituo vya afya Unguja na Pemba kutoa bohari ya dawa.

 Dk. Mwinyi alisema serikali itanunua mitambo ya kuchomea taka za hospitali kwa hospitali zote za wilaya na Mikoa kati ya mitambo hiyo miwili itakuwa na uwezo mkubwa wa kuchoma taka hatarishi ambayo itafungwa katika hospitali za mikoa ili iweze kutoa huduma katika hospitali za karibu za serikali na binafsi. 

 Alibainisha kwamba huduma za damu salama zitaimarishwa kwa kupatiwa vitendea kazi muhimu zinavyoendana na mahitaji husika ili iweze kutoa huduma muda wote.

 Hata hivyo alibainisha kwamba serikali itanunua mitambo miwili katika hospitali za Pangatupu na Abdalla Mzee za kuzalisha gesi tiba kila mmoja ukiwa na uwezo wa kuzalisha mitungi 400 kwa siku itakayotumika kwenye hospitali nyengine Unguja na Pemba zitakazohitaji huduma hiyo.  

 Alisema faida zitakazopatikana baada ya kukamilika miradi hiyo ni kuona huduma bora za afya karibu na wananchi na kutimiza dhamira ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa nje ya Zanzibar kwa ajili ya kufuata matibabu.

 Aidha alisema utwekelezaji wa miradi hiyo mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ya afya katika wilaya zote za Unguja na Pemba ni utekelezaji wa dhamira ya serikali ya tangu Mapinduzi yam waka 1964 ya kuwapatia huduma bora na sahihi za afya wananchi wa Zanzibar.

 SEKTA YA ELIMU

 Kwa upande wa sekta ya elimu Rais Mwinyi alisema serikali imetenga jumla ya bilioni 69 sawa na dola za kimarekani milioni 30 ya fedha za mkopo wa IMF kwa ajili ya kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika sekta ya elimu na kuimarisha kiwango cha elimu inayotolewa nchini.

  Alisema serikali itajenga madarasa 425 yaliyoanzishwa na nguvu za wananchi ambapo shughuli hiyo itagharimu jumla ya shilingi 7.6 na ujenzi wamadarasa mapya 706 katika wilaya zote Unguja na Pemba kwa ngazi ya maandalizi, msingi na sekondari.

  Alisema madarasa hayo yatajumuisha ujenzi wa madarasa mapya nay ale yatakayojengwa kuvutia ujenzi wa skuli mpya 35 zikiwemo skuli 22 za Maandalizi, 13 msingi na sekondari Unguja na Pemba ambapo skuli saba kati ya hizo zitakuwa za horofa.

 Akitaja maeneo yatakayojengwa skuli hizo alisema ni pamoja Mwanakwerekwe, Mtopepo, Bweleo na Kwahani kwa Unguja na Mwambe, Kwale na Makangale kwa kisiwa cha Pemba na skuli mbili katika eneo la Jendele kwa Unguja na Chake Chake kwa Pemba ambazo zitakuwa maalum kwa ajili ya elimu mjumuisho.

  Maeneo mengine ya ujenzi wa skuli hizo alisema ni Mpendae, Kipapo, Pujini na Mgelema ambapo ujenzi huo utagharimu jumla ya shilingi bilioni 43.9.

 Vile vile alibainisha kuwa serikali imeamua kuelekeza jumla ya shilingi bilioni 6.8 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo 1693 vya wanafunzi katika ngazi zote za elimu huku jumla ya bilioni 7.8 zitatumiwa kwa ajili ya ukarabati wa skuli 22 ikiwemo skuli ya Hailesalase, Chaani, Mlemani, Matemwe na Uzini kwa Unguja na Konde, Chasasa na Kiwani Mauwani Pemba.

 Katika sekta hiyo pia alisema serikali itanunua vikalio 8000 kwa skuli ya ngazi ya msingi zitakavyogharimu jumla ya shilingi bilioni 2 sambamba na ujenzi wa nyumba 10 za walimu katika maeneo ya visiwa vidogo vidogo ikiwemo Tumbatu, Uzi, Njao, Kokota na Ngambwa ambapo ujenzi wake utagharimu jumla ya shilingi milioni 600.         

  Alibainisha kwamba serikali itatumia wakandarasi wakubwa wa daraja la kwanza, lapilli na daraja la tatu kuhakikisha ujenzi huo unakuwa wenye ubora unaotakiwa kwani taratibu za kuwapata wakandarasi hao zinaendelea ambapo serikali inatarajia kusaini mikataba na kuanza kwa utekelezaji wa miradi kuanzia mwezi Disemba mwaka huu.  

 Raid Mwinyi alisema gharama zote za ujenzi pamoja na michoro ya majengo ya skuli mpya imeshakamilika kwani serikali ina mafanikio makubwa ya utekelezaji wa miradi yote hiyo ili kuweza kutoa elimu bora kwa watoto ambao ndio warithi wa taifa.  

 Alisema ni imani yake kwamba miradi hiyo ya ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya itachochea sana mzunguko wa fedha kwa kutoa ajira kwa makundi mbalimbali ikiwemo mafundi uwashi, seremala, mama lishe na makundi mbalimbali sambamba na kukuza biashara hasa vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji, nondo na vifaa nyengine.

 SEKTA YA MAJI

 Alisema katika kuzitapita ufumbuzi changamoto zilizokuwepo katika sekta hiyo alisema serikali imetenga jumla ya shilingi 34.2 ambazo zitatumika kwa ajili ya kazi kuu tatu ikiwemo kuongeza uzalishaji wa maji kwa kuchimba visima 28 Unguja na Pemba.

 Aidha alisema visima hivyo vinategemewa kuzalisha jumla ya lita za maji milioni 14.1 kwa siku ambayo shunguli hiyo itatumia shilingi bilioni 2.1 na ununuzi wa vifaa mbalimbali ambavyo vitasaidia katika uchimbaji wa visima ambapo imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 2.1 huku itatumia shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuviendeleza visima 36 Unguja na Pemba vilivyochimbwa kupitia mradi wa Ras alhema ambavyo vinatengemewa kuzalisha lita za maji 15.7 milioni kwa siku.

 Sambamba na hatua hizo alisema pia watafanya ukarabati visima vilivyowekewa pampu chini ya kiwango ambapo jumla ya visima 49 Unguja na Pemba zinategemewa kubadilishwa mashine na kutiwa mashine zenye uwezo unaostahiki kwa mujibu wa uwezo wa visima hivyo ambavyo vinategemewa kuzalisha lita za maji 23.4 milion kwa siku ambapo jumla ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo ni shilingi bilioni 6.9.

 Alisema kupitia fedha hizo serikali imepanga kubadilisha bomba za maji chakavu na kusambaza bomba mpya kwa maeneo ambayo huduma ya maji haijafika ambapo jumla ya kilomita 319 zinategemewa kubadilishwa na kuboreshwa mtandao wa maji ambapo bilioni 8.2 zimepangwa kwa ajili ya kazi hiyo.

 Kadhalika alisema serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 210 kwa ajili ya kukarabati matangi ya maji Unguja na Pemba kwa lengo la kuongeza kiwango cha uhifadhi wa maji ambapo kwa Unguja matangi mawili na Pemba tangi moja yote yakiwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 3.2.

 Alisema pia serikali imetenga shilingi bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa matangi mapya tisa yenye ujazo wa lita milioni 1 kila moja Unguja matangi matano na Pemba matangi manne ambapo jumla ya lita za maji milioni 9.2 zinatarajiwa kuhifadhiwa katika matangi hayo.

 “Kwa kipindi kifupi kijacho tumedhamiria kuongeza kiwango cha maji kutoka lita milioni 131 kwa siku sawa na asilimia 55 hadi lita 170 milioni sawa na asilimia 71 ya mahitaji ya siku kwa wananchi,” alibainisha.

  Dk. Mwinyi alisema serikali itaiwezesha Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa kununua magari mawili ya kuchimba visima kwa Unguja na Pemba.

 SEKTA YA NISHATI

 Kwa upande wa sekta ya umeme alisema serikali imetenga shilingi bilioni 11 kati ya fedha za mkopo wa IMF kwa lengo la kuzitafutia changamoto zilizojitokeza katika sekta hiyo ambapo fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kupunguza gharama za watu wanaotaka kuvuta umeme wananchi wa Unguja na Pemba ambapo wastani wa wateja 30,000 wanatarajiwa kufikiwa.

  Alisema hatua hiyo itajumuisha ujenzi wa miundombinu ya umeme mkubwa pamoja na ununuzi wa vifaa mbalimbali zitakavyotumika katika kazi hiyo ambapo katika mpango huo muombaji wa umeme atachangia shilingi 200,000 badala ya shilingi 600,000 na gharama zilizobaki zitafidiwa na serikali.

  Alifahamisha kuwa lengo la uamuzi huo wa serikali kupunguza gharama za uungaji wa umeme kwa wananchi ni kuwapunguzia gharama hizo ili kuweza kumudu huduma hiyo kwa maisha ya kila siku.

 SEKTA YA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

  Alisema katika kipindi cha kampeni alikutana na makundi mbalimbali kwa ajili ya kujadili maendeleo na kufahamu changamoto zinazowakabili ikiwemo makundi ya vijana, waendesha bodaboda, mama mtilie, wavuvi, wachonga mbao, wafanyabiashara masokoni na makundi mengine.

Rais Mwinyi alisema katika kutatua changamoto ya makundi hayo hasa kukosekana kwa mitaji serikali imetenga shilingi bilioni 85.4 kwa shughuli za uwekezaji wananchi kiuchumi kwa ajili ya kuwaendeleza wajasiriamali hao Unguja na Pemba katika sekta ya uchumi wa bluu na sekta nyengine za uwezeshaji.

 Alisema serikali ya awamu ya nane imedhamiria kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa kutekeleza sera za mipango na kuendeleza uchumi kwa ujumla kwani aliahidi na amedhamiria kutekeleza ahadi alizozitoa kwa wananchi wa Zanzibar.

 Alifahamisha kuwa katika fedha hizo za mkopo amelekeza jumla ya shilingi bilioni 36.5 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wa sekta ya uvuvi na mazao ya baharini.

  Alisema kati ya fedha hizo bilioni 20 zitatumika kwa ajili ya kuwapatia vikundi vya wavuvi boti 577 za kisasa zenye vifaa muhimu vya uvuvi ikiwemo mitengo ya kisasa ya kuvulia na majokofu ya barafu ambapo mpango huo utawanufaisha wavuvi wasiopungua 5,770.

 Rais Mwinyi alisema juhudi kubwa zitaelekezwa katika kuwapatia wananchi na wajasiriamali 31,770 vifaa vya uvuvi na ufugaji wa mazao ya baharini pamoja na usarifu wa dagaa.

 Alisema serikali imetenga bilioni 2.5 kwa ajili ya kuwaendeleza wakulima wa mwani ambapo jumla ya vihori 500 vitanunuliwa hivyo matumaini yake kwamba jumla ya wakulima wa mwani 5,000 watanufaika na mpango huo.

 Alibainisha kuwa shilingi bilioni 1.7 zitatumika kwa aili ya ununuzi wa vifaa kwa ajili ya kuendeleza za hilo na ukamilishaji wa kiwanda cha mwani kisiwani Pemba kwa thamani ya shilingi milioni 500 kwa lengo la kusaidia uogezaji wa thamani ya zao la mwani ili kuongeza tija ya zao hilo.

 Mbali na hayo, alisema serikali imetenga shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kuviwezesha vikundi 100 vya ufugaji wa majongoo ya bahari Unguja na Pemba na jumla ya shilingi milioni 402 zitatumika katika kuendeleza vikubndi 60 vya ufugaji wa kaa na bilioni 1.2 zitatumika kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wanaojishughulisha na ufugaji ambapo jumla ya vikundi 40 vitanufaika na mpango huo.

  Rais Mwinyi alisema fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa bluu ni kuhakikisha zinawanufaisha wananchi 1,580,850 katika myororo mzima wa thamani ambayo ni hatua muhimu katika kutekeleza ahadi ya kukuza ajira nchini.

 Kwa upande wa sekta nyengine za kiuchumi serikali imetega jumla ya shilingi 5.6 kwa ajili ya uwekezaji wajasiriamali wa sekta nyengine ambapo unatarajia kuwanufaisha watu hao na wafanyabiashara wadogo wapatao 101,704 kwa Unguja na Pemba.

 Alisema jumla ya shilingi bilioni 4 zitatumika kwa ajili ya kunufaisha wafanyabiashara wenye viwanda vidogo vidogo na vyakati katika sekta ya useremala, ushoni, utengenezaji wa sabuni, usindikaji wa mazao, viwanda vya kusaga nafaka na viwanda nyengine.

 Hata hivyo alisema jumuiya za waendesha bodaboda kila mkoa watakopeshwa kwa kuanzia bodaboda 50 kwa ajili ya vijana wa mkoa husika hivyo jumla ya wajasiriamali 2,906 waliokuwa katika makundi hayo watanufaika katika mpango huo.        

 SEKTA YA KILIMO NA UFUGAJI

 Rais Mwinyi alisema ni miongoni mwa sekta iliyopewa kipaumbele ambapo litakuwa na miradi 413 ambapo shilingi bilioni 6.7 zitatolewa ambazo zitanufaisha wakulima na wafugaji 8,444.

 Kwa wananchi wanaojishughulisha na kazi za mikono ikiwemo wahunzi, watu wenye ulemavu, wachoraji wa hina, watengenezaji wa mabango, mafundi gereji, wafinyanzi alisema wametengewa jumla ya shilingi bilioni 5 ambazo zitawanufaisha wananchi wapatao 22,600.

 Wafanyabiashara wa maduka ya rejareja na jumuia masokoni, alisema makundi hayo yametengewa shilingi bilioni 5.2 zitakazowanufaisha watu 950 Unguja na Pemba huku bilioni 2.5 kwa ajili ya mama lishe, baba lishe, wamiliki wa mikahawa vijana na watengenezaji simu na vifaa vya umeme kama vile mafriji na kompyuta Unguja na Pemba ambapo idadi ya wanufaika ni elfu 16.

 Alisema sehemu ya fedha hizo pia zitatumika katika ujenzi wa kituo cha kulea na kukuza wajasiriamali ikiwemo kuwapatia mafunzo ya ufugaji wa nyuki ambapo jumla ya wajasiriamali 5,834 ambapo pia katika fedha hizo serikali itaandaa maeneo maalum ya kufanyia biashara kwa wajasiriamali wanaojishughulisha na biashara ya welding, uhunzi na mbao na uchogaji wa thamani ili kuwawekea mazingira mazuri ya biashara.

 Rais Mwinyi alisema hatokata taamaa wala kuvunjika moyo kwa watu wanaomkejeli katika dhamira yake ya uchumi wa bluu kwani wapo wanaofanya kejeli katika dhana hiyo.

 “Nimedhamiria kwani niliyoyasema yote yapo ndani ya dhamira yangu na wahenga wanasema nia njema hairogwi mwaka wa kwanza ulikuwa ukidorora lakini fedha hizi zitaingia katika mzunguko wa uchumi,” alibainisha.

 Aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa fedha hizo zikiingia basi kila mtu atanufaika kwani fedha hizo zitagusa sekta zote hivyo mwaka wa piliwa serikali ya awamu ya nane utakuwa wa mafanikio zaidi.

 Kwa upande wa fedha za mkopo zilizokopwa na serikali bilioni 230 alisema zitatumika kwa ajili ya kuongeza mzunguko wa fedha na wafanyabiashara kwa wananchi ikiwemo ulipaji wa madeni makubwa ambayo serikali inadaiwa nawazabuni, wastaafu, wananchi na wafayakazi wa serikali.

 Alisema serikali imefanya maamuzi kuwalipa wananchi waliowekeza fedha zao katika kampuni ya master life ili kuwasaidia wahanga hao ambao wameathirika na matapeli ambapo shilingi bilioni 6.7 zimepatikana katika akaunti yao.

  Aliwasisitiza wananchi kuendelezxa amani ya nchi yao kwani tayari ndani ya jamii yapo maneno yameanza kuashiria uvujifu wa amani yanayotolewa na baadhi ya viongozi ambao wanataka kuichafua amani iliyopo nchini.

  Hata hivyo aliwasisitiza viongozi kuanzia ngazi ya shehia kuhakikisha wanawajibika katika utekelezaji wa majukumu yao katika kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.

 Akiongea kwa njia ya simu Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wake na kuwataka wazanzibari kushikana kwa pamoja katika kuendeleza umoja amani na mshikamano kwa lengo la kuijenga Zanzibar yao.

 Alisema huu ni mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Mwinyi hivyo ni vyema wananchi wakaendelea kushikamana ili kuifikisha Zanzibar kiuchumi na kimaendeleo.

 Mwenyekiti wa kamati ya sherehe ya kutimiza mwaka mmoja wa uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi Iddrissa Kitwana Mustafa, alisema katika maadhimisho hayo yamefanyika mambo makubwa ikiwemo uzinduzi wa miradi mikubwa na yenye kuleta tija kwa wananchi wa zanzibar.

 Alisema miradi hiyo ilipata nafasi ya kuwekewa mawe ya msingi imeonesha ari ya maendeleo ya serikali ya awamu ya nane kutokana na kasi ya ujezi wake ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tu.