Na mwandishi wetu
Jeshi la Magereza
nchini limepongezwa kwa kubuni utaratibu mzuri wa kujiendesha kimapato kupitia
miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba bora kwa gharama nafuu.
Pongezi hizo zimetolewa
mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti wakati alipozindua
mradi wa nyumba za kuishi askari na mradi wa maji kwenye gereza la kilimo Mollo
Wilaya ya Sumbawanga.
Mkirikiti alifurahishwa
kuona mradi wa nyumba ya kuishi familia mbili iliyojengwa kwa shilingi
Milioni Hamsini na Tano na aliwapongeza
kwa kutekeleza dhana ya Magereza Kujigemea kwa kuwa inaongeza tija kwa mkoa
kupitia miradi inayotekelezwa.
“Kama Magereza imeweza
kujenga nyumba moja ya familia (Two in One) kwa gharama ya shilingi Milioni 57,
huu ni mfano mzuri wa ubunifu. Wito wangu Halmashauri za Rukwa waige mfano huu
kwenye utekelezaji miradi ya ujenzi ili kupunguza gharama za fedha za serikali
“alisisitiza Mkirikiti.
Awali akitoa taarifa ya
miradi, Mkuu wa Gereza la Kilimo Mollo Mrakibu wa Magereza (SP) Nicostratus
Magori alisema mradi wa nyumba za kuishi askari umetekelezwa kwa lengo la
kupunguza uhaba wa makazi bora ya askari .
Aliongeza kusema gharama
halisi za mradi wa nyumba hiyo ni shilingi Milioni 55 ambapo gereza kupitia
miradi yake limechangia shilingi Milioni 17.3 na Kamishna Jenerali wa Magereza
(CGP) alichangia shilingi Milioni 38
Kuhusu mradi wa maji
safi na salama SP Magori alisema jumla ya shilingi Milioni 7.6 imetumika
kufufua mradi huo ambapo fedha zote zimetokana na miradi ya gereza Mollo.
SP Magori alitoa ombi
kwa Mkuu wa Mkoa kuwa gereza lisaidie kupata miradi mbalimbali kwa lina nguvu
kazi na utaalam hatua itakayosaidia kutekeleza miradi kwa ubora huku gereza
likiongeza uwezo wake wa kujitegemea kimapato.
“Miradi hii licha ya
kutuimarisha kiuchumi, inasaidia pia kutoa mafunzo ya ujuzi kwa wafungwa ili
watakapomaliza vifungo vyao itawasaidia kuwa raia wema kwa kufanya kazi halali
za kujitegemea” alisema SP Magori.
Gereza la Kilimo Mollo
lilianzishwa mwaka 1967 ambapo lina eneo la ukubwa ekari 8,989 na kwa sasa lina
miradi ya ujenzi wa nyumba ya kulala wageni, ujenzi wa bwalo, ujenzi wa fremu
11 za maduka na ujenzi wa viwanda vidogo vya kuchaka mazao ya ngano, alizeti na
mahindi.




0 Maoni