Na mwandishi wetu
Serikali ya mapinduzi ya zanzibar itaendelea kutoa msukumo maalum katika kuimarisha miradi ya uwekezaji ili kuwasaidia wawekezaji wazawa na wageni kuendeleza miradi hiyo na kufurahia matunda yanayotokana na uwekezaji huo
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo katika hafla ya uwekaji
wa jiwe la msingi wa mradi wa kiwanda cha maji cha kampuni ya AMOS INDUSTRIES
LIMITED kilichopo chamanangwe mkoa wa kaskazini pemba.
Mhe. Hemed alieleza
kuwa, katika kufanikisha uwekezaji wenye tija Serikali ya awamu ya nane
inayoongozwa na Rais dk.mwinyi imefanya mabadiliko ya sheria nbari 14 ya mwaka
2018 ya kukuza na kumlinda mwekezaji Zanzibar yaliolenga kufungua fursa ya
uwekezaji mkakati kwa upande wa kisiwa cha Pemba.
Alifafanua kwamba,
mabadiliko hayo yametoa fursa kwa muwekezaji anaetaka kuekeza kisiwani Pemba
kuwa na mtaji wa Dola za Kimarekani Millioni Kumi (10) tofauti na kiwango cha
awali kilichokuwepo kwa kumtaka muwekezaji kuwa na kiwango cha Dola Millioni
Hamsini (50).
Alisema miongoni mwa
hatua nyengine zilizochukuliwa na serikali katika kukuza uwekezaji Nchini ni
kukabidhi maeneo tengefu ya aridhi, mashamba ya mipira na visiwa vidogo vidogo
kwa Mamlaka ya kukuza uwekezaji Zanzibar ZIPA kwa lengo la kuimarisha
upatikanaji wa aridhi na kuongeza wigo wa uwekezaji Nchini.
Mhe. Hemed alisema
katika kipindi cha mwaka mmoja kwa serikali ya awamu ya nane tayari jumla ya
miradi Tisini na saba Themanini na saba, Laki Sita ishirini na mbili elfu Mia
moja na sabiini (787,622,170) na nane ishasajiliwa na ipo katika hatua za
utekelezaji.
Katika hatua nyengine
Makamu wa Pili wa Rais alieleza katika kuhakikisha mageuzi ya maendeleo ya
viwanda Zanzibar, serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari imeshakamilisha
utayarishaji wa uchambuzi yakinifu kwa eneo la Micheweni Pemba ambalo litakuwa
chachu kwa uwekezaji na upatikanaji wa ajira kwa wananchi
Kabla ya kumkaribisha
mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais kazi uchumi na uwekezaji Mhe. Mudrik
Ramadhan Soraga alisema azma ya serikali ya awamu ya nane imelenga kufungua
milango zaidi ya uwekezaji ambapo jitihada mbali mbali zimechukuliwa ikiwemo
kufanywa kwa mabadiliko ya sera na sheria.
Mhe. Mudrik alileza
kuwa kutokana na mazingira bora ya uwekezaji yaliofanyiwa marekebisho
wawekezaji wamejenga imani kubwa kwa serikali juu ya usalama wa mitaji yao
wanayoekeza na kueleza kwamba baadhi ya wawekezaji wameanza kurudi kuekeza
Zanzibar.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Mamlaka ya kukuza uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Sharif Ali Sharif
alisema katika kipindi cha mwaka mmoja jumla ya fedha za kitanzania Trilioni
Moja nukta 8 zimetumika katika uwekezaji na jumla ya ajira Elfu Saba (7,000)
zinatarajiwa kupatikana kwa wananchi.
Alisema katika kipindi
hiki cha Mwaka mmoja wa Uongozi wa Dk. MWINYI madarakani ongezeko la miradi
limefikia Mia tatu ishirini na tatu 323 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Nae Mkurugenzi
wa AMOS INDUSTRIES LIMITED Husamudin Ali alieleza kampuni hiyo ya
kizalendo imeamua kuunga mkono jitihada za serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa
kuekeza jumla ya shillingi Billioni Moja nukta nane mpaka utakapokamilika
ujenzi wa kiwanda hicho.
Alieleza kuwa, kiwanda
hicho kinatarajia kuzalisha Maji lita Elfu Tano (5000) ambapo uwepo wa kiwanda
hicho unatarajia kuzalisha ajira kati ya 30 hadi 50 za moja kwa moja na ajira
zaidi ya 60 nje ya kiwanda ikijumuisha kupatikana kwa soko la matunda ya
wakulima kwa ajili ya kutengenezea Juisi.
Pamoja na mambo
mengine Bw. Husamudini Ali aliziomba serikali zote mbili kulipatia ufumbuzi
tatizo la kuzuwiliwa bidhaa zinazozalishwa Zanzibar kwenda Tanzania bara kwa
ajili ya kutanua wigo mpana wa soko la bidhaa za Zanzibar ndani ya Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Katika kuelekea
kipindi hichi cha mwaka mmoja cha Rais Dk. Mwinyi madarakani jumla ya miradi
Kumi na mbili (12) imezinduliwa Unguja na Pemba ambayo inatarajiwa kutoa ajira
kwa wananchi, kukuza uchumi pamoja na kuongeza mapato serikalini kupitia
ukusanyaji wa kodi




0 Maoni