Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Kaskazini Pemba Mgeni Khatibu Yahya
 

Na Mwandishi wetu

Vingozi wa Shehia pamoja na wadau wa maendeleo wa Wilaya ya Micheweni  wametakiawa kuongeza nguvu katika kuandaa mikakati  imara itakayosaidia mradi wa kuwarejesha watoto watoro mashuleni unafanikiwa kikamilifu.

Mkuu wa wilaya ya micheweni, Mh. Mgeni Khatib Yahya ameyasema hayo, katika ukumbi wa Halimashauri ya Wilaya ya  Micheweni Kaskazini Pemba, wakati akizungunza na viongozi wa Shehiya za Wilaya hiyo katika kikao cha Mikakati chenye lengo la kuwarejesha watoro Shuleni

 Amesema  iwapo  viongozi wa shehia watakuwa na ushirikiano baina yao na watu wanaowaongoza katika maeneo yao, jamii  itanufaika vyema katika suala la elimu.

Akijibu hoja za wachangiaji  katika mkutano huo, Afisa mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Nd. Mohamed Nassor Salim,  amesema  kwa upande wao   Wizara ya Elimu iko tayari kuunga mkono jitihada za wadau katika kukamilisha malengo ya mradi huo kwa kutoa elimu kwa  jamii, ili waweze  kushiriki kwa faida ya vizazi Vijavyo.

Akitoa takwimu Afisa Kisomo  Idara ya Elimu Mbadala Pemba, Nd. Haji Juma  amesema,  lengo kuu la elimu mbadala  nikuwarejesha wale wote  ambao  wameacha Shule  na wale ambao hawakusoma.

Nao baadhi ya washiriki hao Sheha wa Shehiya ya Shumba Mjini Rahla Ramadhan na Sharifa Suleiman Mwalimu wa Darasa la Watoto watoro, kutoka Skuli ya Tumbe Msingi, wamesema tayari wameanza utekelezaji wa mikakati katika Shehiya zao  kwani wanaelewa vyema umuhimu wa elimu kwa jamii hasa vijana.