Katibu Mkuu Wizara ya
Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akizungumza na Maafisa
Magereza katika Gereza la Mahabusu Segerea jijini Dar Es Salaam, alipofanya
ziara kwenye gereza hilo.Na mwandishi wetu
Serikali
imewahakikishia wafungwa na mahabusu nchini kuendelea kutatua changamoto
zinazowakabili hususani zinazohusu masuala ya Ustawi wa Jamii wakiwa
magerezani kwa kuzingatia taratibu zote kama ilivyo kwa makundi mengine.
Hayo yamebainishwa leo
jijini Dar Es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya
Jamii, Dkt. John Jingu katika ziara yake ya kikazi kwenye Gereza la Mahabusu ya
Segerea.
Akizungumza mara baada
ya ziara hiyo, Dkt. Jingu amesema kuwa ziara hiyo imekuwa ya
mafanikio kwake na wataalam alioongozana nao na imewafumbua macho juu ya
utendaji kazi ndani ya gereza, changamoto zinazowakabili mahabusu na wafungwa
na namna ya kuzitatua.
Katika ziara hiyo Dkt.
John Jingu amekiri kujifunza mambo mengi yatakayoiwezesha Wizara kuboresha
utendaji kazi wake hususan makundi inayoyasimamia yakiwemo wanawake na
watoto na kuhakikisha changamoto zinazowakabili wakiwa mahabusu
na wafungwa zinatatuliwa.
“Tumekuwa na ziara za
aina hii katika magereza mbalimbali nchini na tutahakikisha tunafika katika
magereza yote na tunatafuta namna bora zaidi ya Ustawi wa Jamii wa makundi ya
wafungwa na mahabusu katika magereza wakwiemo Wanawake na Watoto waliokinzana
na Sheria” alisema Dkt. Jingu.
Ameongeza kuwa makundi
hayo ni sehemu ya jukumu kubwa la Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya
Jamii ambayo inasimamia masuala ya Jinsia, Wazee na Watoto na maendeleo kwa
ujumla wake hivyo, ziara za aina hiyo zinaongeza uelewa kuhusu masuala
yanayoendelea katika maeneo kama haya ya magereza.
“Tumejifunza mambo
mengi kutoka kwa wahusika hawa, na uelewa huu utatuwezesha kuboresha utendaji
kazi wetu kama Wizara na pale kwenye matatizo ya kijamii tunajengewa uwezo
kuhusu namna kupata ufumbuzi wa matatizo ya kijamii kwa matendo badala ya
kuongozwa na nadharia” alisisitiza.
Aidha, ameitaka jamii
kujitafakari kuhusu matendo yanayosababisha wanajamii kujikuta wanakinzana na Sheria
na wakati mwingine kutafuta mbinu za kuepusha migogoro ya kijamii ili
kujiepusha kuangukia gerezani.
Akiwa katika Gereza
hilo, Katibu Mkuu Jingu alipata fursa ya kuzungumza na mahabusu waliochini ya
miaka 18 (watoto), pamoja na mahabusu na wafungwa wanawake.
Akizungumzia ziara ya
Katibu Mkuu katika Gereza la Segerea, Mkuu wa Gereza Msaidizi Gereza hilo,
Mrakibu wa Magereza, Athanas Ndowano amesema kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa
Ustawi na Maendeleo ya Jamii na inaweza kuboresha na kurahisisha utekelezaji wa
majukumu yao.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akitoka katika Gereza la Mahabusu, Segerea Jijini Dar es Salaam mara baada ya ziara yake Gerezani hapo, kushoto kwake ni Mkuu wa Gereza Msaidizi, Gereza la Mahabusu Segerea , Mrakibu wa Magereza, Athanas Ndowano na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Lucy Saleko.




0 Maoni