wameambatana
na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi.
Na mwandishi wetu
Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, imeainisha vipaumbele
vitakavyonufaika na mradi wa sekta ya afya kwa kipindi cha miaka mitatu kwa
ufadhili wa Serikali ya Italia.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee Prof.
Abel Makubi amevibainisha vipaumbele hivyo alipokutana na madaktari kutoka
Italia leo Jijini Dar es Salaam ambapo vipaumbele hivyo ni mafunzo kwa
wataalamu wa afya katika hospitali za mkoa, kanda na Taifa kwa ujumla, kununua
vifaa vya matibabu vya kisasa, kujenga na kukarabati hospitali za kanda na
taifa.
“Vipaumbele vingine ni kuanzisha na kuendeleza ushirikiano katika sekta ya afya kati ya Tanzania na Italia, kuimarisha mifumo ya maabara katika hospitali na kuendelea kupambana na ugonjwa wa Uviko 19 ikiwa ni pamoja na kuelimisha umuhimu wa chanjo” amesema Prof. Makubi.
Kwa upande wake Balozi wa Italia hapa nchini,
Mhe. Marco Lombardi amelipongeza Shirika la Maendeleo la Italia kwa kutenga
Euro 1,250,000 za msaada wenye manufaa kwa sekta ya afya nchini.
“Ushirikiano baina ya Tanzania na Italia ni wa muda mrefu na imara,
naomba nikuhakikishie kuwa Italia itaendelea kushirikiana na Serikali ya
Tanzania katika sekta ya afya pamoja na sekta nyingine kwa maslahi ya pande
zote mbili na kwetu sisi kama Italia huu ni mwanzo na tunaamini kuwa kupitia
mradi huu uhusiano wetu utaendelea kuimarika zaidi,” amesema Balozi Lombardi.
Nae Dkt. Davide Bonechi, Daktari kutoka Kituo cha Taifa la Italia cha
Afya Duniani amesema kuwa kupitia mpango wao wa kuboresha na kuimarisha sekta
ya afya katika ukanda wa Afrika, mbali na Tanzania nchi nyingine zitakazo
nufaika na mpango huo ni Kenya na Uganda.
“Lengo letu ni kuboresha sekta ya afya kwa ujumla pamoja na
kuwaongezea uwezo wataalamu wa afya ili waweze kukabiliana na magonjwa
mbalimbali yanayowapata binadamu,” amesema Dkt. Bonechi
Tarehe 3 September ujumbe wa wataalam wa afya kutoka nchini Italia
uliwasili Tanzania kwa ziara maalum ya kutathmini na kufahamu mahitaji na
vipaumbele vya Tanzania katika ya afya kwa hospitali zilizopo nchini.
Ujumbe wa wataalam wa afya kutoka nchini Italia unaongozwa na Dkt.
Davide Bonechi, Dkt. Giulia Dagliana, pamoja na Dkt. Beatrice Borchi, wote
wakitoka katika Kituo cha Taifa la Italia cha Afya Duniani.
Tanzania imekuwa
ikishirikiana na Italia katika miradi mbalimbali ya afya hapa nchini ambapo
ushirikiano rasmi katika sekta ya afya ulianza mwaka 1968 kupitia Shirika la
Madaktari wa Italia-CUAMM-Doctors with Africa. Kuanzia wakati huo, Serikali ya
Italia imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya afya hapa nchini kama vile miradi
ya kupambana na utapiamlo,
afya ya watoto wachanga, afya ya uzazi na kupunguza maambizi ya virusi vya
ukimwi.
Serikali ya Tanzania imekuwa
ikipokea madaktari wa binadamu na wataalamu wa dawa za binadamu kutoka Italia
ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa kutoa huduma za matibabu.





0 Maoni