Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema pamoja kuwa tozo za miamala ya simu zimepunguzwa kwa asilimia 30 lakini tozo hizo ni muhimu kwa kuwa zinachangia upatikanaji wa huduma muhimu za jamii
Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe
02 Septemba, 2021 wakati aliposimama kuwasalimia wananchi wa Tegeta Jijini Dar es Salaam na Zinga, Bagamoyo
mkoani Pwani wakati akielekea Bagamoyo mjini kuendelea kurekodi vivutio
mbalimbali vya utalii katika kipindi
maarufu cha Royal Tour.
Amesema Serikali imeamua
kuweka tozo hiyo kwa dhamira ya kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali za
huduma ambapo katika kipindi cha miezi miwili Serikali kupitia tozo hizo
imejenga vituo vya afya 220 pamoja na ukamilishaji wa madarasa 560 katika
maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewahakikishia
wananchi hao wa Tegeta (Dar es Salaam) na Zinga (Bagamoyo) kuwa miradi yote ya
kimkakati iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano inakamilika kama
ilivyokusudiwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM pamoja na
miradi mingine mipya.
Akizungumzia ujenzi wa
mradi wa Bandari ya Bagamoyo, Mhe. Rais Samia amesema mradi huo ni mkubwa na
Serikali kwa sasa inaupitia upya ili ijiridhishe kwasababu utasaidia kutoa
ajira na kukuza uchumi wa pamoja na kuboresha huduma za kijamii.
Kuhusu UVIKO 19, Mhe. Rais Samia amewataka
wananchi kuona umuhimu wa kupata chanjo kwani ugonjwa huo bado upo na
unaendelea kupoteza maisha kwa wananchi.
Mapema Mbunge wa Jimbo la Kawe Mhe. Askofu
Josphat Gwajima, Mhe. Ridhiwani Kikwete Mbunge wa Chalinze na Mhe. Muharami
Mkenge Mbunge wa Bagamoyo wamempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada mbalimbali
anazofanya katika kuwaletea maendeleo wananchi na kuahidi kuendelea
kushirikiana naye.







0 Maoni