RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwahutubia Wananchi wa Wilaya ya
Chakechake Pemba katika ufunguzi wa jengo jipya la Bodi ya Mapato Zanzibar
(ZRB) lilioko katika eneo la Gombani Pemba, hafla hiyo ya ufunguzi imefanyika
katika viwanja vya jengo hilo Na mwandishi wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi amesema kuwa ujenzi wa jengo jipya la Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB)
Pemba ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuimarisha mazingira mazuri ya
kufanyia kazi kwa watumishi wa umma ili kuongeza ufanisi katika utendaji na
utoaji huduma kwa wananchi.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo katika uzinduzi wa Jengo jipya la Bodi ya
Mapato Zanzibar (ZRB), huko Gombani, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Kisiwani Pemba.
Katika hotuba yake Rais Dk. Mwinyi amesema kazi kubwa imefanywa na Serikali
ya Awamu ya Saba katika kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi kisiwani Pemba
ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Ofisi za Serikali zilizopo Gombani, Jengo jipya la
ZSSF pamoja na majengo mengine mengi ambapo kila Wizara ina ofisi ya kisasa
kisiwani Pemba.
Amesema kuwa majengo ya kisasa yaliyojengwa sio tu kwamba yana mchango
mkubwa katika mazingira ya kufanyia kazi bali pia yanaongeza taswira ya mji
pamoja na kuufanya mji uwe wa kupendeza.
Ameongeza kuwa ujenzi wa ofisi za kisasa ni hatua muhimu katika utekelezaji
wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa ni eneo maalum la kimkakati la uwekezaji
sambamba na kuhakikisha kwamba huduma na mahitaji muhimu kwa wananchi na
wawekezaji yanayopatikana Unguja pia, yapatikane kisiwani Pemba.
Ameeleza umuhimu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato (ZRB) kufanya kazi kwa pamoja, na kusema kwamba kuwepo kutoa huduma Pemba kutasaidia wananchi.
Nae Waziri wa Fedha na Mipango Jamali Kassim Ali alisema kuwa jengo hilo lina mambo yote muhimu ya kufanyia kazi na kuweza kuwarahishia kuweza kutoa huduma bora kwa wateja hasa wale walipa kodi.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi Dk. Juma Maliki Akil, alisema kuwa jengo hilo linachochea kuleta utulivu wa kufanyia kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Pia, jengo hilo kutokana na miundombinu yake kutakuwa na usalama wa kutosha na ulinzi pamoja na utunzaji bora wa kumbukumbu wa nyaraka kutokana na mfumo mliojengwa wa tehama katika jengo hilo.
Pia, litakuwa na kitengo cha dharura, na kuwa na huduma za kuaminika hasa
huduma za umeme ambapo litakuwa na umeme muda wote hata pale huduma hiyo
ikikosekana.
Jengo hilo lina ghorofa nne, ghala, na sehemu nyenginezo ambapo kuanzia ghorofa ya kwanza hadi ya nne kuna vyumba kwa ajili ya wafanyakazi mbali mbali , pamoja na kuwepo kumbi mbali mbali.
Sambamba na hayo, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa mkataba wa ujenzi wa jengo
hilo ulitiwa saini mwezi Disemba 2019 kati ya ZRB na Mkandarasi ‘Advent
Construction Limited’ ambaye ni kutoka Dar-es-Salaam .na kukamilika rasmi mwezi
Mei mwaka 2021 kwa gharama za TZS Bilioni 10.6.




0 Maoni