Serikali ya Omani inatarajia kutoa msaada wa kifaa cha kuangalia Mwezi mwandamo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuiwezesha ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kutumia teknolojia katika shuhuli za utafutaji wa Mwezi kama ilivyo katika mataifa mengine yaliyoendelea.

Kifaa hicho kinatarajiwa kufika mwaka huu kabla ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Hayo yamesemwa na Balozi Mdogo wa Oman, Said Salum Al-sinawi katika Ofisi ya Mufti wa Zanzibar iliyopo Mazinizi Mkoa wa Mjini Magharib alipofika ofisini hapo kwaajili ya  kujitambulisha kufuatia Balozi aliokuwepo awali kumaliza mda wake.

Amesema Zanzibar na Serikali ya Omani ni watu wenye udugu wa damu kwa mda mrefu, hivyo ipo haja ya kuisaidia katika kila nyanja ya maendeleo.

“Mimi naelewa kuwa Zanzibar na Oman ni ndugu wa damu tutakuwa pamoja ili kuendeleza udugu wetu” alisema Balozi huyo.

Amesema anacho kifanya hivi sasa ni kuangalia maombi yote yaliyofika mezani katika ubalozi huo ambayo yamepangwa kutekelezwa na Balozi aliepita na kuyapa umuhimu na kuyafanikisha kwani hilo ndio jukumu lake .

“Nimeona maombi yenu mara tu kufika Ofisini ni jambo jema nitashughulikia hilo ni masuala muhimu kuweza kutekeleza”, aliongeza kusema balozi huyo.

Amesema ameyaona maombi yao yapo mezani ikiwemo maombi ya uendelezaji wa ujenzi wa Ofisi ya mufti,kifaa chakuangalizia mwezi na mambo mengine mengi ambayo ni muhimu.

”Nimeona maombi na nitayafanyia kazi na hichi kifaa chakuangalizia mwezi kitafika kabla ya Mwezi mtukufu wa Ramadhani”,alisema Balozi Ali Salum.

Nae Mufti wa Zanzibar sheikh Saleh Omar Kabi, alimshukuru kiongozi huyo kwa ujio wake kufika ofisini hapo na kusema ujio huo ni kuendeleza udugu wao wa damu ambao Zanzibar inafaidika sana na Misaada ya Serikali ya Omani ikiwemi ujenzi wa Misikiti,nyumba za kihistoria,vyuo na maeneo mengine ya kijamii.

Mufti huyo alisema, Omani iendelee kuisaidia Zanzibar na isiishie hapo kwani misaada yao imekua ni chachu ya kuendeleza masuala ya dini ya kislamu katika visiwa vya Zanzibar hivyo ni muhimu sana kuona dini ya kislamu inasimamiwa misingi yake.

Aidha mufti huo alisema kuwa wao wako tayari kuendelea na kuisimamia ofisi hiyo kwa nia safi ili kuendeleza uislamu na kusimamia taratibu zake.