Uongozi wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi umetakiwa kuweka utaratibu mzuri wa kuwahudumia wananchi wanaofika kupata huduma katika Idara ya Usafiri na Leseni.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameeleza hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani iliyopo Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi ‘’B’’ Unguja.

Amesema Serikali inahitaji mapato katika uendeshaji wa kazi zake hivyo mamlaka hiyo ina jukumu la msingi la kuweka utaratibu imara utakaosaidia kuingizia serikali mapato, ili kusaidia kukuza uchumi wa Nchi.

Akizungumzia juu ya suala la kughushi nyaraka feki Mhe. Hemed alimuagiza Mkurugenzi Mkuu Mamlaka Usafiri na Usalama barabarani kuchukua hatua kali dhidi ya watu watakaobainika kufanya vitendo hivyo ikiwemo kuwafikisha mahakamani ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo kuangalia namna bora ya kuimarisha ulinzi katika eneo la maegesho ya magari kwa kufunga Kamera za usalama ili kudhibiti uhalifu unaojitokeza mara kwa mara.

Aidha, aliwataka wananchi wanaofika kupata huduma katika mamlaka hiyo kujenga tabia ya uaminifu na kauchana na vitendo vya utapeli ikiwemo kughushi nyaraka za Serikali ili kujenga mashirikiano mazuri na wafanyakazi wa idara hiyo.

Akijibu baadhi ya changamoto zilozotolewa na wananchi Mkurugenzi Mkuu mamlaka ya Usafiri na Usalama barabarani Haji Ali Zubeir alisema mamlaka anayoisimamia imekuwa ikichukua hatua kwa wananchi wanaokiuka taratibu ili kuondosha vitendo vya kihalifu ikiwemo kughushi nyaraka feki za Leseni.

Ameeleza kuwa, mamlaka ya Usafiri na Usalama barabarani imekuwa ikisimamia sheria kwa wanafunzi wanaojifunza udereva kwa kutumia gari za manual badala ya automatic ili kuwajengea umahiri wanafunzi hao na kupunguza idadi ya ajali na athari mbali mbali wanapokuwa Barabarani.