Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe:Ayoub Mohamed Mahmoud ameishauri kamati ya Sensa ya Mkoa huo kuzingatia vipaumbele  vya  huduma  za Jamii watakapoanza kuhesabu Watu na Makaazi yao.

Akizindua Kamati hiyo Ofisini kwake Mkokotoni Mhe: Ayoub amesema sensa ni kwaajili ya ustawi wa  jamii  hivyo kutozingatia upatikanaji wa huduma za jamii ni kurejesha nyuma maendeleo ya wananchi.

Amesema Serikali imeamua kufanya Sensa ni kwaajili ya kupanga huduma  kwa jamii hivyo kushindwa kutambua huduma inayohitajika Kwa Sehemu husika  itasababisha Serikali Kushindwa Kupanga Miundombinu ya huduma kwa sehemu hiyo jambo ambalo ni kuwakosesha Wananchi kupata haki yao ya msingi.

Mjumbe wa kamati hiyo Ndugu Sabri Muhoma amesema Sensa ya mara hii itakuwa na madadisi manne yatakayozingatia huduma za jamii, idadi ya Kaya, Majengo Na  Anuani Za Makaazi hivyo amewataka wananchi kujiandaa na sensa hiyo ili lengo la Serikali  Lifanikiwe.

Sensa ya  watu na makaazi inayotarajiwa kufanyika Mwaka 2022 Na Majaribio Ya Sensa Hiyo Itafanyika Tarehe 11 Mwezi Huu Na Kwa Upande Wa Mkoa Wa Kaskazini Unguja Shehiya Ya Kilindi Na Shehia Ya Bumbwini Misufini Zitahusika Na Sensa Hiyo Ya Majaribio.