WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa yote nchini wasimamie miradi ya maendeleo na uzalishaji wa mazao kulingana na jiografia ya maeneo husika.

 Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi, Agosti 12, 2021) wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote na Kamati zao za Ulinzi na Usalama kuhusu usimamizi wa miradi ya maendeleo kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya video (video conferencing) kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

 “Asilimia 75 ya wananchi kwenye mikoa yenu, wanajishughulisha na kilimo. Lazima Ma-RC tusimamie kilimo huko tuliko. Kwa kawaida tunalima kwa kutegemea mvua lakini kwenye mikoa ambayo ina mito, ni vema tugeukie kilimo cha umwagiliaji maji kwa kutumia gharama kidogo,” amesema.

 “Kule wilayani, maafisa kilimo wahusishwe kwenye miradi ya umwagiliaji, ingawa tumeunda Tume ya Umwagiliaji pekee, lakini tunahitaji maafisa kilimo wasimamie miradi yote na wahakikishe inafanya kazi.”

 Kuhusu mazao ya kimkakati, Waziri Mkuu amesema imeendelea kusimamia mazao kama alizeti, chikichi, parachichi na sasa inaimarisha mazao ya ufuta, kokoa na fiwi. Amewataka wakuu hao wa mikoa wasimamie mazao hata kama kuna changamoto ya bei.

 “Ni lazima tulime hata kama kuna changamoto ya bei, msimu ukianza kila mmoja lazima ajihusishe na kilimo. Ukichukulia zao la alizeti, utabaini kuwa lina uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya viwanda. Iweje sasa, viwanda vinafungwa kwa kukosa malighafi?”

 Ameyataja maeneo mengine ambayo yanahitaji usimamizi wa karibu kuwa ni miradi ya ujenzi wa barabara, umeme vijijini, elimu, maji, afya na ulinzi na usalama. “Miradi ya barabara iwe ni ya TANROADS au TARURA, isimamieni, mjue iko mingapi, imekamilika au la na kama imekwama tafuteni kujua sababu zilizofanya ikwame. Ni wajibu wenu kuhakikisha inakamilika kwa wakati,” amesisitiza.

 Kuhusu usambazaji wa umeme vijijini, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inataka ifikapo Desemba, 2021 iwe imemaliza kupeleka umeme kwenye vijiji 1,900 vilivyobakia na ianze kupeleka kwenye vitongoji.

 Amewataka wakuu hao wasimamie wakandarasi walioko kwenye mikoa yao na kujiridhisha ujenzi wa miradi hiyo umefikia hatua zipi. “Hatuwezi kuwaacha wawe wanajenga kwa spidi wanayotaka wao kwani tunataka ifikapo mwaka 2025 nchi nzima iwe inawaka taa,” amesema.

 Kuhusu elimu, Waziri Mkuu amewataka wakuu wa mikoa wasimamie fedha zinazotumwa kutoka TAMISEMI na Mamlaka ya Elimu nchini (TEA) ili kuhakikisha kuwa zinafanya kazi katika muda uliopangwa. “Fedha ikija haipaswi kukaa zaidi ya wiki, ni lazima ziende kwenye maeneo ya utekelezaji,” amesisitiza.