Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mhe. Selemani Jafo (mbele) akiwa na Meneja wa Kanda ya mashariki kaskazini Bw. Anorld Mapinduzi wakati wa
ukaguzi wa mazingira kwenye kiwanda cha Sayona kinachomilikiwa na Kampuni ya
Motison Group.Na mwandishi wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mhe. Selemani Jafo ametoa miezi sita kwa wamiliki wa kiwanda Cha
Sayona kinachomilikiwa na Kampuni ya Motison Group ambacho kinazalisha bidhaa
za plastiki, rangi na Chuma kuhakikisha kinatenga eneo maalumu la kuhifadhia
bidhaa za vinywaji ili kuepuka kuchanganyika na bidhaa zisizo za chakula zinazo zalishwa kiwandani
hapo.
Waziri Jafo ameyasema katika ziara yake kwenye kampuni ya Motison Group
inayomilikiwa na kampuni ya Sayona,
Mikocheni Jijini Dar es Salaam.
"Kiwanda hiki mmejitahidi kwenye mfumo wa
kutibu maji, lakini tatizo nililolibaini ni kwamba mnaweka bidhaa za vinywaji
sehemu moja na bidhaa nyingine kama
rangi na plastiki jambo ambalo ni hatari kwa afya zetu. Ninatoa miezi sita
kuanzia sasa mtenge sehemu maalumu ya kuhifadhia bidhaa za vinywaji ili kuepuka
madhara ya kiafya ya mtumiaji wa vinywaji mnavyozalisha hapa."
Katika hatua nyingine Waziri Jafo amekataa kusaini
kibali cha kukusanya chuma chakavu kwenye kiwanda cha Iron & Steel
kilichopo Mikocheni Jijini Dar es salaam mpaka kitakapoweka mfumo mzuri wa
kuzuia moshi usisambae angani.
Waziri Jafo amechukua hatua hiyo baada ya kupokea
malalamiko kutoka kwa wakazi walio karibu na kiwanda hicho kutoa moshi unaoleta
athari kwa afya zao.
" Viwanda vinatoa ajira kwa Wananchi wetu,
mbali na hilo vinalipa kodi kwa Serikali yetu. Pamoja na hizi faida ni lazima
tuzingatie utunzaji wa mazingira yetu. Kiwanda hiki hakina mfumo mzuri wa kutoa
moshi jambo ambalo ni hatari kwa afya ya wakazi wa eneo hili, hivyo naagiza
wafanye marekebisho ili wapate kibali cha ukusanyaji wa vyuma chakavu."
amesema Waziri Jafo.




0 Maoni