Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Mkuya Salum amewataka wazazi na walezi
kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora ili
kuwajenga katika msingi wa maadili mema.
Akizungumza na
wanafunzi pamoja na wajumbe katika Kongamano la Tuongee Faraja Club (TFC)
lilioandaliwa na walimu na wanafunzi wa Skuli ya Faraja katika ukumbi wa
Skuli hiyo amesema wazazi wasiridhike na matokeo wanayopata watoto maskulini
bali wafuatilie na mienendo yao.
Amesema kuwa,
uanzishwaji wa Club hiyo utasaidia kushajihisha wanafunzi kuwa na maadili mema
ambao ndio msingi wa maendeleo ya jamii pamoja na kusaidia kupunguza vitendo
vya udhalilishaji nchini.
“Vitendo vya
udhalilishaji ni vingi katika jamii yetu ni vyema tukiwa mstari wa mbele katika
kuwalea watoto katika maadili mema pamoja na kupingana na ukatili huu,
nawapongeza walimu na wanafunzi kwa kuanzisha Clubu hii ambayo ina lengo la
kupinga vitendo vya udhalilishaji” alisema Waziri huyo.
Aidha aliwaasa
wanafunzi wa Skuli ya hiyo kuwa watiifu kwa walimu wao na kuiendeleza Club hiyo
yenye lengo la kuisaidia Serikali katika kupinga na Vitendo vya Ukatili na
Udhalilishaji wa kijinsi.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Udhibiti na Uchunguzi Tume ya Dawa za Kulevya Juma Abdul-rahman
Zidikheiry ameitaka jamii ijiepushe na vitendo hivi vya matumizi ya madawa ya
kulevya ili kuilinda nguvu kazi ya taifa isipotee.
Aidha amesema Serikali
inaendelea kupanga sheria madhubuti ya kudhibiti dawa za kulevya ili kutokomeza
uhalifu huu, kwani ni kosa kujihusisa na ushiriki wa aina yoyote ikiwa kwa
kuvuta, kuuza, kununua na mengineyo.
Akizungumzia kuhusu
maambukizi ya virusi vya Ukimwi Mwakilishi kutoka Tume ya Ukimwi, Halima Ali
Mohamed amesema vijana wengi kuanzia umri wa miaka 15 hadi 35 wamekuwa ni
waathirika wakubwa wa maradhi ya Ukimwi kutokana na kujihusisha na vitendo ya
uasharati katika umri mdogo.
Alieleza kuwa
kushamiri kwa vitendo vya ulawiti, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na
mporomoko wa maadili unachangia kwa kiasi kikubwa katika kusababisha maambukizi
ya Virusi vya Ukimwi.
Aliwashauri wazazi na
walezi pamoja na walimu kuwa karibu na wanafunzi ili kuweza kutatua changamoto
zinazowakabili wanapokuwa nje ya mazingira ya nyumbani au Skuli ili kuepusha
uwezekano wa kupata magonjwa ikiwemo Ukimwi.




0 Maoni