Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema vitendo vya ukeketaji vinaendelea nchini kwakuwa wnaume hawajaamua kuukataa.
Akizungumza Wilayani Tarime Mkoa wa Mara
alipotembelea kituo Nyumba Salama cha Masanga kinachotumika kuwalea watoto
waliokumbwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia au walio katika hatari ya
kukumbwa na vitendo hivyo.
Dkt. Gwajima amesema ukeketaji unaweza kukomeshwa
nchini endapo wanaume watakaa katika makundi yao na kujadiliana jinsi ya
kukomesha vitendo hivyo.
Hata hivyo amesema wakati umefika kwa jamii kuachana
na visingizio vinavyosababisha kuendelea kwa vitendo vya unyanyasaji wa
kijinsia kwa wanawake na watoto na badala yake kusimamia misingi ya upatikanaji
wa haki.
Awali Meneja wa Mradi wa kupinga Ukeketaji Kituoni
hapo, Valerian Mgani amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya bweni,
chombo cha usafiri na watoto wa kike kukatishwa masomo, kukeketwa na ndoa
katika umri mdogo.
Kituo cha Nyumba salama cha Masanga kilianzishwa
mwaka 2006 na kusajili mwaka 2015 kwa lengo la kuwahudumia watoto wahanga wa
ukatili ukiwemo ukeketaji ambapo hadi sasa kituo hicho kinahudumia walengwa 34
kati yao mmoja ni wa kiume.




0 Maoni