Katika kukabiliana na uvuvi haramu Visiwani Zanzibar,
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Abdallah Hassan amesema Serikali inakusudia
kuwawezesha wavuvi kwa kuwapa vifaa vitakavyowawezesha kuvua kwenye kina kirefu
cha maji.
Akizindua kamati ya wavuvi wa eneo la hifadhi za
Bahari ya Visiwa vya Changuu Bawe, amesema hatua hiyo itasaidia kulinda
Mazingira ya Bahari, kuzuwia Uvuvi haramu na kuchochea Uvuvi wenye tija.
Ameeleza kuwa Wizara imeunda kamati hiyo ili wawe
mabalozi kwa wavuvi ambao hadi sasa wanaendelea kuvua uvuvi haramu.
Aidha Mhe. Abdallah ameitaka kamati hiyo inayoundwa
na wavuvi wa Madiko mbalimbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi kuhakikisha mapato
yanayokusanywa kwa wavuvi yanawafikia walengwa ili kuepusha udanganyifu.
Nae Mkurugenzi wa idara ya uhifadhi wa bahari, Dkt. Makame
Omar amesema hifadhi ya Bawe na Changuu ina rasilimali muhimu kwa maendeleo ya
uvuvi wa utalii ikiwemo Samaki, Mikoko na Majongoo.
Hata hivyo amesema rasilimali hizo zinatoweka
kutokana na athari mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, uchafuzi wa
mazimgira na uchomaji mkaa. Amezitaka kamati hizo kukabiliana na athari hizo
ili kuweka mazingira mazuri ya bahari.





0 Maoni