Waziri Afya Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia  na Watoto Zanzibar Nassor Mazrui amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya,  tayari wameanza kutoa chanjo ya Covid 19 kwa watu  9,350 kutoka  katika makundi maalumu ambayo yako hatarini kuambukizwa ugonjwa  wa covid 19.

  Waziri Mazrui ametoa kauli hiyo August 11 wakati akitoa tamko la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kuhusu hali ya ugonjwa wa Korona Zanzibar , katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mnazi mmoja Mkoa wa Mjini Magharib.

 Amesema  idadi hiyo ya watu ni katika kipindi cha kuanzia tarehe 17 Juni 2021 hadi kufikia August 10, 2021 ambapo kati yao jumla ya watu 5,447 wameshakamilisha dozi na watu 3,903 wanasubiri tarehe waliopangiwa kukamilisha dozi zao.

 Waziri Mazrui ameyataja wakundi yaliyopewa kipaumbele  ni pamoja na wafanyakazi wa milango mikuu ya kuingia nchini ikiwemo Viwanja vya Ndege na Bandarini, wadau wa utalii wakiwemo waongoza watalii, madereva wanaosafirisha wageni na watalii

 Katika taarifa hiyo ameyataja makundi mengine yaliyopewa kipaumbele  kua ni wafanyakazi wa vyombo vya usafiri vya ndani na nje ya nchi, wafanyakazi wa mahoteli, wazee kuanzia umri wa miaka 55 na watu wenye magonjwa sugu na magonjwa ya  muda mrefu.

 Katika hatua nyingine Waziri Mazrui amezitaja Chanjo zilizoruhusiwa na Serikali kutumika hapa Nchini ni chanjo ya Sinovac na Sputnik Light 5 ambazo tayari zimeanza kutolewa.

 Amesisitiza kuwa tokea chanjo ilipoanza kutolewa hadi kufikia sasa hakuna mtu alielazimishwa au  atakaelazimishwa  kuchanja chanjo hiyo kwani wapo baadhi ya madktari ambao hawakuchanja kwakua ni jambo la hiari

 Hata hivyo ameyataja maeneo yanayotolewa chanjo hizo  ni kitengo cha kupambana na kudhibiti maradhi ya miripuko kilichopo  Lumumba na Hospitali ya Mnazi mmoja lakini chanjo hizo zitatolewa katika vituo vyengine ikiwemo hospitali Kivunge,Makunduchi, Abdalla Mzee,Wete na hopitali ya Chake Chake.