SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema jumla ya watu 390 wamegundulika kuwa na maambukizi ya Virusi vya korona hapa Zanzibar wakiwemo watanzania 112 na wageni 278 ambao walitoka katika mataifa mbali mbali duniani.

 Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, alitoa kauli hiyo wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu kuwepo kwa wagonjwa wa korona hapa Zanzibar ambao unasambaa kwa kasi kubwa Ofisini kwake Mnazimmoja.

 Alisema wagonjwa hao ni kati ya watu 29,326 waliopimwa Virusi vya Corona (COVID-19) katika vituo na Hospitali mbalimbali Unguja na Pemba kuanzia Juni 25 hadi Agosti 10 mwaka huu .

  Alisema kati ya wagonjwa hao 390 waliothibitika, watu 207 wamepona na wagonjwa waliobaki 183 wakiwemo watanzania 32 na wageni 151 huku wagonjwa 24 wamelazwa na wanaendelea na matibabu katika Hospitali mbali mbali hapa Zanzibar.

 Waziri huyo alibainisha kuwa kuanzia mwezi Juni hadi August, 2021 jumla ya vifo 15 vya wazanzibari vilitokea vilisababishwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19) na kuripotiwa katika hospitali mbalimbali hapa nchini.

 Alibainisha kuwa Zanzibar inakabiliwa na ugonjwa huo huku serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo hapa Zanzibar.

 Akizungumzia chanjo ya Korona amesema wizara inaendelea na hatua mbali mbali za kinga dhidi ya ugonjwa huo ikiwemo utoaji wa chanjo.

 Waziri huyo amesema kwa sasa wameanza kutoa chanjo ya korona kwa makundi maalumu ambayo ni hatarishi zaidi kuambukizwa ugonjwa huo.

 Akiyata makundi hayo alisema ni pamoja na wafanyakazi wa milango mikuu ya kuingia nchini ikiwemo viwanja vya ndege na bandarini, wadau wa utalii wakiwemo waongoza watalii, madereva wanaosafirisha wageni na watalii, wafanyakazi wa vyombo vya usafiri vya ndani na nje ya nchi, wafanyakazi wa mahoteli, wazee kuanzia miaka 55 na watu wenye magonjwa sugu na ya muda mrefu.