Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah anatarajiwa kuwa mgeni rasmi siku ya Uzinduzi wa Wiki ya mwananchi iliyoandaliwa na Klabu ya Yanga inayotarajiwa kuzinduliwa Asubuhi ya   Jumapili Agost 22 2021

Sambamba na Sherehe nyengine  Uzinduzi huo pia utahusisha Dua ya kumuombea Muasisi wa Klabu hiyo ambae pia ndie Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza na Wanahabari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Hamasa, Qs. Suma Mwaitenda amezema Uzinduzi huo wa Wiki ya Mwananchi utaambatana na shughuli mbalimbali za Kijamii zikazofanywa na Wana Yanga Sc na viongozi wa Yanga Sc.

"Tutakuwa na shughuli za kijamii kuanzia  Jumamosi (leo), tunatarajia kuwa tutatoa msaada wa mgodoro katika Hospitali za Mnazi Mmoja na Mwemberadu, lakini Jumapili ndio utakuwa uzinduzi rasmi ambao utafanyika baada ya dua maalum ya kumuombea muasisi wetu, Hayati Sheikh Abeid Aman Karume," amesema.

Amesema Jumapili Wana Yanga Sc watakusanyika ofisi za Yanga Sc Kariakoo Zanzibar  na kisha kufanya matembezi ya mshikamano kwenda Ofisi ya CCM Kisiwandui lilipo kaburi la Marehemu Karume ambapo itafanyika Dua

"Katika matukio yote ya Dua na baadaye Uzinduzi kwenye ukumbi wa ZSSF mgeni wetu tunataraji atakuwa Makamu wa Pili wa Rais," amesema.

Katika hatua nyingine, Qs. Suma Mwaitenda ameishukuru Kampuni ya Azam Marine and Kilimanjaro Fast Ferries kwa kujitokeza kuwa mmoja wa Wadhamini wa Wiki ya Mwananchi mwaka huu.