Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amemwambia naibu wake William Ruto ajiuzulu, badala ya kuendelea kuikosoa serikali yake. Rais Kenyatta pia amesema hakukubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali kesi ya BBI lakini amesema ataheshimu uamuzi huo.

Uhuru aliongeza kuwa alishangaa kwanini naibu wake alikuwa akipinga mchakato wa BBI akisema "maswala yaliyopelekea kuundwa kwa BBI ndio yaleyale yaliyowaleta pamoja".

Hii ndio mara ya kwanza kwa rais Kenyatta kufunguka kuhusu mwenendo wa Naibu wake ambaye tayari ameshasema anataka kuwania urais mwaka 2022 kupitia chama kipya cha UDA.

Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya Habari nchini Kenya, rais Kenyatta amesema anashangazwa na mwenendo wa naibu wake ambaye anapinga mipango ya serikali ambayo anaitumikia.

Rais Kenyatta amesema hakuwa na shida na Ruto kujenga ngome yake kisiasa lakini alihoji njia ambazo timu ya UDA inatumia.