Madiwani wa halmashauri ya Kishapu Mkoani Shinyanga wameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo yao ili kuwaondolea wananchi adha ya kulazimika kutumia mikokoteni  ya Ng’ombe kusafirishia wagonjwa  hasa kipindi cha masika kutokana na uchakavu wa miundombinu ya Barabara.

Hayo wameyasema agost 27, 2021  kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo, ambapo wamesema hali ya barabara inayotoka Migunga, Mwataga kwenda Isoso wakati wa masika hazipitiki hivyo huwaweka hatarini wananchi ambao ni wagonjwa kwa kubebwa katika magaria ya Ng’ombe kwaajili ya kupelekwa Hospital.

Diwani wa Kata ya Mwataga halmashauri ya Kishapu  Mhe Matungwa Daudi na diwani wa Kiloleli wamesema hali hiyo inapelekea wagonjwa wengine kupoteza maisha wakiwa wapo njiani kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya uhakika ya barabara na usafiri

'Tunaiomba serikali itusaidie juu ya hili kutokana na barabara kuwa mbovu hazipitiki mwaka juzi kuna mama mmoja alipoteza maisha kutokana na kukosekana kwa barabara, hivyo tunaomba barabara zitengenezwe ili kunusuru afya za wananchi,amesema Daudi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo amesema kero za barabara zinaonekana zipo kila kata hivyo Tarura iliangalie vizuri suala hili kwani wananchi wanahitaji barabara waweze kupata matibabu kwa muda na waweze kusafirisha mazao yao kwa wakati.

Kwa upande wake Meneja wa Tarura Wilaya ya Kishapu Samson Pamphili amesema serikali ilikuwa imetenga Sh 800.9  milioni lakini baada ya kuona changamoto za barabara ni nyingi iliongeza fedha ikafika Sh 2.4 Bilioni ambazo zimeelekezwa kuishirikisha halmashauri na mbunge, na fedha hizo zimeelekezwa kwenye barabara ambazo hazipitiki kabisa zipewe kipaumbele.