Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesitisha Leseni ya Uchapishaji ya Gazeti la Uhuru kwa muda wa siku Kumi na Nne kuanzia tarehe 12 Agosti,2021

Taarifa ya kusitishwa Uchapaji wa Gazeti hilo imetolewa na Idara ya Habari Maelezo katika taarifa yake kwa waandishi wa habari ambapo taarifa hiyo Imeeleza uamuzi huo unatokana na Gazeti hilo toleo Na 24084 katika ukurasa wa mbele kuchapisha habari inayosomeka ‘Sina wazo kuwania urais 2025 – Samia’, habari ambayo imeendelea ukurasa wa pili.

‘‘Kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu cha 9(b) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016 nimeamua kusitisha kwa muda wa siku kumi na nne (14) leseni ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la UHURU kuanzia tarehe 12 Agosti, 2021’’.

Taarifa hiyo imeeleza kua Ofisi ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, imebaini kuwa habari hiyo ina upungufu wa kisheria na weledi wa taaluma ya Uandishi wa Habari  kwa kutoa taarifa za uongo dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kinyume na kifungu cha 50(1)(a),(b), na (d)  na kifungu cha 52(d) na (e) vya Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016. Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan hajatoa matamshi yoyote ambayo yanaeleza kutokuwa na wazo la kuwania urais mwaka 2025.

Pia, kwa mujibu wa kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016, ikiwa gazeti la UHURU halitaridhika na uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari linayo haki ya kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya Habari.