Na mwandishi wetu
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amelitaka Baraza la tiba asili Zanzibar
kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaofanya biashara holela za tiba
hizo bila ya kusajiliwa.
Mhe. Hemed alitoa wito
huo katika maadhimisho ya kumi na tisa ya siku ya tiba asili Barani Afrika
yaliyofanyika leo Agost 31,2021 katika Ukumbi wa Rahaleo Mkoa wa Mjini
Magharibi.
Amesema kwamba sio
jambo la kuridhisha kutokana na wimbi kubwa la waganga wasiosajiliwa kutoa
huduma za tiba asilia katika misikiti, masoko pamoja na maeneo mengine ya wazi
jambo ambalo linahatarisha usalama wa afya za wananchi.
Katika hatua nyengine
Mhe. Hemed aliwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kuwa makini na
kuachana na tabia ya kununua dawa kiholela, dawa ambazo hazijafanyiwa utafiti
na kuthibitishwa na mamlaka husika.
Amewataka wataalamu
hao wa tiba asilia kuitumia vyema fursa waliyonayo katika jamii kwa kuacha
kusababisha migongano miongoni mwa jamii pamoja na kuepuka vitendo vya
udhalilishaji kwa watu wanaofika kwao kupata tiba hizo.
Amesema kuwa kitendo
cha kuitumia vibaya fursa waliyonayo ya kutoa huduma ya tiba asili kwa wananchi
itasabisha kuharibu taswira nzima ya tasnia ya tiba asilia Tanzania na barani
Afrika kwa ujumla.
Nae Waziri wa Afya
Usatwi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amelitaka Baraza
la tiba asili na tiba mbadala Zanzibar kuendelea kushirkiana na wizara
anayoiongoa kwa lengo la kukuza tiba hiyo, hasa kuona namna bora ya kuanzisah
maabara kwa ajili ya kuchunguza dawa asili ili dawa hizo ziwe na viwango sahihi
kwa matumizi ya binadamu.
Amesema tiba asili
zina mchango mkubwa katika kuisaidia Wizara ya Afya kwa kuwapatia tiba wananchi
wa Zanzibar, hasa kwa kuwapatia wagonjwa huduma ya kwanza mara tu wanapopata
tatizo la kiafya..
Akitoa salamu za Shirika
la Afya ulimwenguni (WHO) mwakilishi wa Shirika hilo Dk. Simon Verndelin amesema
shirika hilo limefurahishwa na maamuzi ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungani wa
Tanzania katika kupambana na Uviko 19 kwa kuwataka wataalamu wa tiba asilia
kujumuika pamoja na wataalamu wengie, kwa lengo la kutoa ushauri wao katika
kukabiliana na janga hilo.
Amesema Shirika la
Afya Duniani kwa kutambua mchango wa tiba asili limendelea kuwaunga mkono
wataalamu wa tiba hizo kwa kutoa kila aina ya msaada ikiwemo rasilimali fedha
kwa ajili ya kufanikisha kazi za wataalamu hao Nchini.
Akisoma Risala Kaimu
Mrajisi wa Baraza la Tiba asili Zanzibar Ndugu Muhamed Mshenga Matano, ameeleza
kuwa, Baraza limekuwa likiwafahamisha na kuwaelekeza zaidi waganga wa tiba
asilia kujua namna bora zitakazoweza kuboresha huduma zao ili ziwe na viwango
sahihi vya matumizi pamoja na kuendana na kasi ya kukuwa kwa teknolojia.
Bw. Matano alisema
Baraza limekuwa likifanya kazi kubwa ya kuwaunganisha Waganga kwa kutumia njia
ya kuendesha semina elekezi pamoja na mikutano mbali mbali lengo ikiwa kupata
nguvu kazi ya pamoja katika kutoa huduma kwa wananchi.
Ameeleza kuwa, tangu
Baraza hilo lianzishwe mwaka 2006 limekuwa likifanya ukaguzi na limefanikiwa
kuwakagua waganga 624, maduka 156, pamoja na Kliniki mbali mbali.
Alisema pamoja na jitihada hizo walizozichukua lakini bado kumekuwa na muitiko mdogo kwa baadhi ya waganga kujitokeza na kusajiliwa na baraza hilo jambo linalopelekea waganga wengi kufanya kazi bila kufuata taratibu.





0 Maoni