Wafanyabiashara Nchini
wametakiwa kuacha mara moja upandishaji wa bei za bidhaa ili kuwapunguzia
wananchi ukali wa maisha.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo katika kikao maalum
kilichowakutanisha Viongozi wa wizara,wafanyabishara, na maafisa wa usimamizi
wa Kodi kwa lengo la kulipatia ufumbuzi tatizo la upandaji wa Bei za Bidhaa.
Mhe. Hemed alisema sio
jambo linapendeza kwa wafanyabiashara kukiuka miongozo na taratibu zilizowekwa
na serikali juu ya bei za bidhaa kutokana na upandishaji wa bei unasababisha
usumbufu mkubwa kwa wananchi hasa wale wa kipato cha chini.
Alieleza kuwa wananchi
wamekuwa wakiitupia lawama serikali yao kwa kuona hakuna unafuu wa bidhaa hasa
za chakula jambo linalosababishwa na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.
Katika kikao Hicho
Makamu wa Pili wa Rais alilazimika kupiga simu kwa wauzaji wa bidhaa kutoka Nje
ya Nchi ili kulinganisha gharama za bei wanazonunulia wafanyabiashara hao na
bei wanazowauzia wananchi na kugundua kuwa kuna tofauti kubwa ya bei hizo.
Aliwataka
wafanyabiashara hao kupunguza bei za bidhaa mara moja kabla serikali
haijachukuwa hatua za kinidhamu dhidi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu
kwa kuwafutia kibali cha kufanya biashara Zanzibar.
Akichangia katika
kikao hicho Waziri wa Biashara na maendeleo ya viwanda Mhe. Omar Said Shaaban
alimuleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa na tabia ya
kukacha kufuata miongozo inayowekwa na serikali katika udhaaji wa bei za
bidhaa.
Kwa Upande wake Waziri
wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe. Jamal Kassim Ali alisema kuwa
wananchi wa Zanzibar hawana jukumu la kuwachangia Mitaji wafabyabiashara katika
kuendesha biasgara zao, hivyo suala la kupandisha bei za bidhaa bila ya kufuata
taratibu halikubaliki.
Nae, mfanyabisha
maarufu Zanzibar Said Bopar aliwataka wafanyabishara wenziwe kuwa waaminifu kwa
kuwaonea huruma wananchi kutokana na upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko
kuwa wa kuridhisha.
Katika kikao hicho
kilichowakutanisha wadau kutoka sekta mbali mbali kimetoka na azimio kwa bei ya
dumu moja la mafuta liuzwe kwa bei ya Shillingi Sabiini na Tano Elfu (75,000/=)
kutoka Shilling Themanini na Mbili Elfu ikiwa ni tofauti ya shilling Elfu saba.





0 Maoni