Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar imedhamiria kuimarisha utendaji kazi serikalini kwa kuwachukulia
hatua watendaji wote wasio wajibuka ipasavyo katika majukumu yao ya kazi.
Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo jana (August
10) alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha Damu salama kilichopo
Sebleni Amani Kwa wazee.
Alileza kuwa, wapo
watendaji wazembe wasiopenda kutekeleza majukumu katika sehemu zao za kazi
jambo ambalo halileti ufanisi hivyo serikali itachukua hatua kwa lengo la
kuimarisha utendaji katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katika hatua nyengine
Mhe Hemed amesema Kituo cha damu salama kina umuhimu mkubwa katika kuokoa
maisha ya watu hivyo kuna kila sababu kwa watendaji wake kufanya kazi kwa
uwadilifu na uwaminifu ili kufanikisha lengo lililokusudiwa.
Akikagua maabara
maalum ya kuchunguza na kuhifadhia damu Makamu wa Pili wa Rais alimtaka
msimamizi wa maabara hiyo kuwa makini katika kuhakikisha damu hizo
zilizochangiwa kwa hiyari na wananchi zinahifadhiwa kwa umakini mkubwa.
Aidha, katika
kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizowasilishwa na wafanyakazi Mhe. Hemed
alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Wiazra ya Afya Dk. Abdalla Suleiman kuzichukua
changamoto hizo na kupitia uongozi wa Wizara ya Afya angalie namna bora ya
kuzipatia ufumbuzi.
Pamoja na mambo
mengine Makamu wa Pili wa Rais hakuridhishwa na utaratibu wa kuzihifadhi taka
katika kituo hicho huku akimuagiza Mkurugenzi Mkuu huyo kuwasilisha taarifa
kamili juu ya kuharibika kwa kifaa maalum cha Kuchomea taka ili kuepuka kuzaga
kwa taka katika maeneo yasiokuwa rasmi.






0 Maoni