Katibu
Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel
(katikati) akiongea na Ujumbe kutoka nchini Saudi Arabia alipokutana nao
jijini Dar es Salaam leo Agosti 7, 2021. Kushoto kwake ni Mkaguzi, Mamlaka
ya Dawa na Chakula, Saudi Arabia, Ahmed Alhajouj.Na Mwndishi wetu
Katibu Mkuu, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel amekutana na Ujumbe kutoka nchini
Saudi Arabia kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara ya nyama
na nchi hiyo.
Prof. Ole Gabriel
alikutana na Ujumbe huo kutoka Saudi Arabia ulioongozwa na Mkaguzi, Mamlaka ya Dawa na Chakula, Saudi Arabia,
Ahmed Alhajouj jijini Dar es Salaam Agosti 7, 2021.
Kwa mujibu wa Prof.
Gabriel kabla ya kukutana nao, ujumbe huo ulipata fursa ya kukagua maeneo
mbalimbali yanayohusika na uchakataji wa mazao ya mifugo ikiwemo Machinjio,
Maabara na Shirika la Viwango Tanzania(TBS) ambapo kote wamejirisha na kutoa
mapendekezo kadhaa ya kuboresha ili biashara hiyo iweze kufanyika kwa viwango
vinavyohitajika na nchi hiyo.
Alisema kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameielekeza Wizara
hiyo kutafuta masoko nje ya nchi hivyo Wizara inaendelea kufanya jitihada
ikiwemo hatua hiyo ya kutafuta soko katika nchi Saudi Arabia.
"Haya masoko ya
nje ya nchi ni mazuri kwa sababu yanatupatia fedha za kigeni lakini pia
yanawahakikishia wafugaji wetu soko la uhakika kwa mazao ya mifugo yao,"
alisema Prof. Ole Gabriel
Aidha, Prof. Gabriel
alitoa rai kwa Wafugaji nchini kuchukulia hatua hiyo kama ni fursa kubwa na
hivyo wahakikishe wanaboresha ufugaji wao kuwa wa kisasa zaidi ili kukidhi soko
hilo la kimataifa.
Alisema Sekta ya Mifugo
kwa sasa inachangia katika pato la Taifa kwa asilimia 7.4 lakini lengo la
Wizara ni kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2025 na hilo linawezekana kama
milango ya masoko nje ya nchi ikianza
kufunguka kwa uhakika.
Naye, Msajili wa Bodi ya
Nyama, Dkt. Daniel Mushi alisema anaishukuru Serikali kwa jitihada mbalimbali
inazozifanya kwa kushirikiana na wadau kufungua masoko mengine nje ya nchi ili
kuuza nyama katika masoko yanayolipa bei nzuri.
Itakumbukwa hivi
karibuni, Rais Samia alikutana na Mtoto wa Mfalme wa Saudi Arabia ambapo
miongoni mwa maeneo yaliyoangaliwa ni pamoja na Sekta ya Mifugo na aliielekeza
Wizara kutafuta masoko nje ya nchi ikiwemo nchi ya Saudi Arabia.




0 Maoni