Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 16 Agosti, 2021
amewasili Lilongwe nchini Malawi kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 41 wa Wakuu
wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
utakaofanyika tarehe 17 – 18 Agosti,2021.
Mara baada ya kuwasili
katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kamuzu, Mhe. Rais Samia amepokelewa na
Mhe. Patricia Kaliati, Waziri wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Malawi.
Katika Mkutano huo wa 41
wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC, Jamhuri ya Malawi itathibitishwa kuwa
Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja (Agosti 2021 – Agosti 2022)
Aidha, Wakuu hao wa Nchi
na Serikali watamthibitisha Katibu Mtendaji mpya wa SADC baada ya Katibu
Mtendaji aliyepo Dkt. Stergomena Tax kumaliza muda wake baada ya kuhudumu kwa
ufanisi nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka nane.
Wakuu hao wa Nchi na Serikali wa SADC pia wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ya Mtangamano pamoja na kuidhinisha kauli mbiu ya Jumuiya hiyo.







0 Maoni