Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan, ameitaka jamii nchini kulinda na kuendeleza mila, tamaduni na
desturi zilizo nzuri na kuwarithisha vizazi vya sasa na vijazvyo.
Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 28 Agosti,
2021 wakati akihutubia kwenye kilele cha Tamasha la Kizimkazi katika Kijiji cha
Kizimkazi kusini Unguja Zanzibar.
Amesema kwa sasa dunia ipo kwenye zama za utandawazi
hivyo mikakati thabiti inahitajika kuhakikisha jamii inalinda mila, tamaduni na
desturi zilizo nzuri ili zisipotee na kuachana na zile mbaya kama ndoa za
utotoni na ukeketaji.
Mhe. Rais Samia amesema pamoja na mambo mengine,
Tamasha la Kizimkazi linahamasisha miradi ya maendeleo kufanyika ikiwemo ujenzi
na ukarabati wa shule za awali, Msingi na Sekondari, nyumba za walimu pamoja na
nyumba za watumishi wa afya.
Lengo jingine la Tamasha hilo ni kutangaza fursa za
kiuchumi zilizopo kwenye eneo hilo hususan kilimo, utalii, uchumi wa bahari ama
uchumi wa buluu na utalii wa pomboo (Dolphin)
ambao hupatikana katika eneo hilo la Kizimkazi.
Vilevile, Mhe. Rais Samia amewahimiza wananchi
kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika mwezi
Agosti mwaka 2022, kwa kuwa Sensa ni muhimu katika kuwezesha Serikali kufahamu
idadi ya watu itakayosadia kupanga mipango ya maendeleo.
Mhe. Rais Samia amewataka wananchi kuendelea
kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO 19 na kujitokeza kupata chanjo katika
kukabiliana na maradhi hayo.
Katika kilele cha Tamasha hilo Mhe. Rais Samia
ametembelea mabanda ya Wajasiriamali na kujionea bidhaa wanazozalisha, kuzindua
majengo mbalimbali, kupokea maandamano ya vijana takribani 250 na kushuhudia
maonesho ya asili ya Shomoo.
Mhe. Rais Samia amewashukuru wafadhili waliochangia
miradi ya maendeleo na kufanikisha
kufanyika kwa Tamasha hilo ikiwemo Benki ya CRDB, NMB, NBC, Kampuni na Mshirika
mbalimbali pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan, akiondoa kitambaa kuzindua rasmi Nyumba za Madaktari na Jengo la Ofisi
ya Maendeleo Kizimkazi katika Tamsha la Kizimkazi zilililofanyika leo tarehe 28
Agosti 2021 katika Kijiji cha Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.







0 Maoni